WANUFAIKA TASAF WANOLEWA JUU YA MATUMIZI YA NISHATI MBADALA

Wanufaika wa mfuko wa kusaidia kaya maskini TASAF wameshauriwa kutumia nishati mbadala ikiwemo majiko sanifu na gesi ili kuepukana na matumizi makubwa ya kuni na mkaa yanayoathiri uoto wa asili na mabadiliko ya tabianchi
Hayo yamebainika leo tarehe 03 Februari,2025 wakati wa zoezi la malipo ya fedha za mfuko wa kunusuru kaya maskini TASAF kwa dirisha la Novemba -Disemba 2024 lililofanyika katika Kijiji cha Mgaraganza kilichopo kata ya Kagongo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Afisa Maendeleo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Bw.George Vangisauli amesema umefika wakati sasa kwa wananchi kuhamia kwenye nishati ya gesi kwa kuwa itawawezesha kuokoa muda na gharama kubwa ukilinganisha na nishati ya kuni na mkaa.
"Ninaomba tuhamie kwenye gesi,haya ndio maendeleo,ule muda unaotumia kwenda porini kutafuta kuni au mkaa ni bora ukautumia kufanya shughuli nyingine za uzalishaji mali" amesema Bw.Vangisauli
Baadhi ya wanufaika wa mfuko huo licha ya kuipongeza Serikali kwa kuendelea kusambaza huduma ya umeme vijijini, wameshauri umeme uendelee kusambazwa kwenye maeneo ambayo bado kwa kuwa uwepo wa huduma hiyo utapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi hasa ya kuni.
"Nyakati za usiku tumekua tukalizimika kutumia mienge ya moto kumulika ili kupata mwanga,lakini umeme ukiwepo tunaweza kufanya shughuli zetu kwa urahisi hasa nyakati za usiku"amesisitiza mnufaika mmojapo kutoka kijiji cha Mgaraganza
Malipo ya fedha za mfuko wa kunusuru kaya maskini kwa dirisha la Novemba -Disemba 2024 yanaendelea kufanyika katika vijiji mbalimbali vya Halmashauri ya wilaya ya Kigoma huku elimu kuhusu matumizi ya nishati mbadala ikipigiwa chapuo ili kuunga mkono jitihada za Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. follow *** kigomadcofficial***