SERIKALI YAKABIDHI MABOTI MAWILI YENYE THAMANI YA TSH MILIONI 100 KWA AJILI YA KUIMARISHA DORIA ZIWA TANGANYIKA

Serikali kwa kushirikiana na Shirika la FISH 4 ACP imekabidhi maboti mawili yenye thamani ya shilingi milioni 100 kwa vikundi vya Beach Management Unit (BMU) vilivyopo katika Kata ya Mtanga na Kata ya Kagunga, Wilaya ya Kigoma, ikiwa ni jitihada za kuimarisha doria na kudhibiti vitendo vya uvuvi haramu katika Ziwa Tanganyika.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Afisa Uvuvi wa Halmashauri hiyo, Bw. Kilenga Williamu, amesema upatikanaji wa maboti hayo ni hatua muhimu katika mapambano dhidi ya uvuvi haramu na kwamba yatasaidia kulinda rasilimali za uvuvi, kuongeza ubora wa mazao ya samaki na kuinua kipato cha wavuvi wa eneo hilo.
“Maboti haya ni nyenzo muhimu za kuhakikisha doria zinafanyika kwa ufanisi. Lengo letu ni kumaliza kabisa changamoto ya uvuvi haramu na kuhakikisha sekta ya uvuvi inachangia kikamilifu maendeleo ya jamii na uchumi wa Taifa,” amesema Bw. Williamu.
Kupatikana kwa maboti haya ni sehemu ya juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha uvuvi endelevu na usimamizi bora wa rasilimali za Ziwa Tanganyika, ambalo ni chanzo kikuu cha kipato na lishe kwa maelfu ya wakazi wa Kigoma na maeneo jirani.