CHMT KIGOMA DC YAFUATILIA KWA UKARIBU HUDUMA ZA AFYA MWAMBAO WA ZIWA TANGANYIKA

Timu ya Usimamizi wa Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma (CHMT) Imefanya ziara ya usimamizi shirikishi katika vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoko mwambao mwa Ziwa Tanganyika kwa lengo la kubaini changamoto na kuboresha huduma kwa wananchi wa maeneo hayo.
Ziara hiyo imefanyika, Leo 4 Septemba 2025 imehusisha ukaguzi wa huduma katika vituo vya Kigalye, Mtanga, Mwamgongo Health Center, Bugamba, Kiziba, Zashe, Kagunga na Gombe, sambamba na utoaji wa huduma za afya kwa wananchi waliotembelea vituo hivyo.
Huduma zilizotolewa ni pamoja na chanjo mbalimbali, upimaji wa afya, ushauri wa afya kwa jamii, upimaji wa Virusi vya Ukimwi (VVU), na upimaji wa malaria.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Dkt. Aswile Mwambembe, amesema kuwa usimamizi shirikishi ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya karibu na makazi yake.
"Kupitia usimamizi shirikishi, tumepata nafasi ya kujionea hali halisi ya utoaji huduma na changamoto zilizopo, sambamba na kutoa huduma moja kwa moja kwa wananchi, hatua itakayosaidia kupanga mikakati madhubuti ya maboresho," amesema Dkt. Mwambembe.
Viongozi wa vijiji vilivyotembelewa wamepongeza juhudi za Serikali za kufuatilia kwa karibu hali ya utoaji huduma za afya, wakieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi wanaoishi maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau wa afya na jamii ili kuhakikisha huduma bora za afya zinaimarishwa na kufikishwa kwa wananchi wote bila kujali umbali au mazingira wanayoishi.