JESHI LA MAGEREZA KWITANGA LAFANYA USAFI HOSPITALI YA WILAYA YA KIGOMA LIKIFANYA MAADHIMISHO YA WIKI YAKE

Mkuu wa Jeshi la Magereza ya Kwitanga ACP Eleck John Nkete katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma pamoja wamefanya Maadhimisho ya wiki ya Jeshi hilo kwa kufanya zoezi la usafi katika Hospitali ya Wilaya ya Kigoma leo tarehe 25 Agosti,2025.
Mkuu wa Jeshi la Magereza ya Kwitanga amesema lengo la kufanya zoezi hilo ni kuendelea kudumisha mashirikiano mema baina ya jamii na Jeshi hilo ili kusaidia kurekebisha tabia za wahalifu kwa kushirikiana na Jamii ikiwemo makundi,taasisi au mashirika mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma,Katibu wa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Bi.Asha Mwingira licha ya kulishukuru jeshi hilo kwa kushiriki zoezi la usafi ametoa mwito kwa wadau au makundi mengine kuendelea kushirikiana na Hospitali ya Wilaya kwenye masuala mbalimbali ili kuendelea kuboresha utoaji wa huduma.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Dkt.Lidya Msofe amesema zoezi lililofanywa na jeshi hilo ni la kupigiwa mfano na kulishukuru jeshi hilo kwa kufanya usafi kwenye eneo kubwa kwa muda mfupi jambo ambalo limeendelea kuboresha mandhari ya Hospitali na usafi kwa ujumla.
Jeshi la Magereza kote nchini linafanya Maadhimisho ya Wiki yake yenye Kaulimbiu "Ushirikiano wa Jeshi la Magereza na Jamii kwa urekebishaji wenye tija"yaliyoanza tarehe 23 Agosti 2025 ambapo yanatarajiwa kufikia Kilele chake tarehe 26 Agosti,2025.