NG’OMBE 7,000 KUCHANJWA DHIDI YA HOMA YA MAPAFU KIGOMA DC

Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma imezindua rasmi zoezi la chanjo kwa ng’ombe 7,000 kwa Kata zote 16 ili kudhibiti ugonjwa wa homa ya mapafu (CBPP) unaoathiri mifugo na kuathiri uzalishaji wa sekta ya mifugo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bw. Mustapha Magembe, amesema lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha mifugo inalindwa dhidi ya magonjwa, kuongeza uzalishaji, na kuimarisha kipato cha wafugaji.
“Tunatoa wito kwa maafisa mifugo kuhakikisha chanjo hii inatolewa kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali. Wafugaji wanahimizwa kushirikiana na wataalamu wetu kwa kutoa mifugo yao kwa ajili ya chanjo ili kulinda afya za mifugo na kipato chao,” amesema Bw. Mustapha Magembe.
Mbali na utoaji wa chanjo, zoezi hilo litakwenda sambamba na utambuzi na usajili wa mifugo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, hatua inayolenga kuimarisha takwimu sahihi za mifugo na uboreshaji wa huduma za sekta hiyo.
Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma umeeleza dhamira yake ya kuendeleza sekta ya mifugo kwa kuhakikisha mifugo inapata huduma bora za kinga na tiba, ili kuongeza mchango wake kwenye uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.