WAKAZI ZAIDI YA ELFU 30 KUTOKA KATA ZA KALINZI,MKIGO NA NYARUBANDA KUONDOKANA NA ADHA YA UMBALI MREFU KUTAFUTA HUDUMA YA AFYA

Wananchi zaidi ya Elfu 30 kutoka Kata za Kalinzi,Mkigo na Nyarubanda wanatarajiwa kunufaika na huduma ya afya baada ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kalinzi uliogharimu thamani ya shilingi milioni 500 kukamilika na kuanza kutoa huduma.
Hayo yamebainika leo tarehe 7,Machi 2025 Baada ya Mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini Mhe.Assa Makanika kuzindua majengo matano ya Kituo cha Afya cha Kalinzi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kilichojengwa kwa nguvu ya Wananchi na fedha za Serikali kuu.
Kituo hicho cha Afya ambacho kina jengo la Idara ya wagonjwa wa nje,jengo la Maabara,jengo la Upasuaji pamoja na wodi ya Wazazi inaelezwa kuwa ni mafanikio ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Afya inayoelekeza kila Kata kuwa na Kituo cha Afya kitakachotoa huduma karibu zaidi na makazi ya Wananchi.
Akizungumza na Wananchi baada ya uzinduzi, Mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini Mhe.Assa Makanika amesema pamoja na Ujenzi wa Kituo hicho tayari Serikali imeleta vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 100 kwaajili ya kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Dkt.Robert Manyerere amesema wanamshukuru Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati ya kupunguza vifo vya Mama na mtoto na kuamua kupeleka fedha nyingi ili vituo vya afya vijengwe kwaajili ya kuwasaidia Wananchi.
Kituo cha Afya cha Kalinzi ni miongoni mwa vituo vya Afya ambavyo tayari vimejengwa kwenye kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwa lengo la kuwapunguzia Wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya afya.