VIJANA ZAIDI YA ELFU 17 KIGOMA D.C KUNUFAIKA NA KILIMO-BIASHARA KUPITIA MRADI WA YEFFA

Vijana zaidi ya Elfu 17 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wanaojihusisha na shughuli za kilimo wanatarajia kunufaika na mafunzo, mitaji, na masoko ili kujiingizia kipato kupitia kilimo cha tija.
Hayo yamebainika leo tarehe 15 Agosti 2025 kwenye uzinduzi rasmi wa mradi mpya wa YEFFA(Youth Entrepreneurship for Future of Food and Agriculture) uliofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwa kushirikiana na Shirika la SOGECO na AGRA kwa ufadhili wa Mastercard Foundation.
Mradi huo mpya wa YEFFA ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu (2024–2027) ukilenga kuibua fursa mpya, kuongeza thamani ya mazao, na kuboresha maisha ya vijana kupitia ubunifu na ujasiriamali wa kilimo utajikita kwenye mazao ya alizeti, mazao ya bustani, mahindi, mpunga na maharage.
Akizungumza katika uzinduzi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Rasilimali Josephat Kataga amesisitiza kuwa hii ni nafasi ya kipekee kwa vijana wa Kigoma Tanzania kwa ujumla, wenye ndoto na dhamira ya kujiendeleza kupitia kilimo chenye tija.
Mradi huu unalenga kuwajengea uwezo vijana zaidi ya milioni 6.9 katika mikoa saba ya Tanzania ikiwemo Kigoma,Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Ruvuma ili kujiajiri kupitia kilimo-biashara chenye tija na thamani.