VIKUNDI VYA WANAWAKE,VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU KUPEWA ELIMU YA FEDHA KUHUSU MIKOPO YA ASILIMIA 10
Posted on: October 21st, 2024Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigoma Bw.Mganwa Nzota amewaasa Maafisa maendeleo kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa vikundi vya Wanawake,vijana na Watu wenye Ulemavu wanaopewa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwaajili ya kuviwezesha vikundi hivyo kujiinua kiuchumi.
Katibu Tawala Nzota ametoa kauli hiyo leo tarehe 21 Oktoba,2024 kwenye Mafunzo kuhusu mikopo inayotolewa kwenye vikundi vya Wanawake vijana na Watu wenye Ulemavu yaliyoshirikisha Wakuu wa Vitengo na Idara mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma pamoja na Maafisa Maendeleo wa Mkoa wa Kigoma na Wajumbe wengine mbalimbali.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amerejesha mikopo ya asilimia 10 ili kuwainua Wananchi hasa makundi ya Wanawake vijana na Watu wenye Ulemavu ambapo jumla ya Shilingi 200,380,614/=zimetengwa katika Robo ya Pili ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 kwaajili ya Mikopo hiyo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
DAS Nzota ameongeza kuwa umri wa Vijana wanaopaswa kuomba mikopo umeongezwa kuanzia miaka 18 hadi 35 tofauti na awali ili kuwapa fursa vijana wengi zaidi kupata mikopo na kujishughulisha na shughuli zitakazowaingizia kipato.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Bw.Jabir Timbuka amesema Halmashauri imejipanga vizuri katika kuhakikisha fedha ya mikopo ya asilimia 10 inatolewa kwa walengwa wote na kuandaa utaratibu mzuri utakaowarahisishia vikundi vya Wanawake vijana na Watu wenye ulemavu kupata fedha hiyo ya mikopo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.