UZINDUZI WA UTEKELEZAJI WA MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI HALMASHAURI YA WILAYA YA KIGOMA

Uzinduzi wa utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi umezinduliwa tarehe 24 Machi, 2022 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mh. Ester Alexander Mahawe. Uzinduzi huo uliambatana na kikao kazi ili kutoa maelekezo kwa Watendaji wa Kata na Vijiji kuhusu utekelezaji wa zoezi hilo. Kikao kazi hicho kimeudhuriwa pia na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wakiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Mh. Joseph Nyambwe, Waheshimiwa Madiwani na Wakuu wa Idara mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Katika hotuba yake, Mh. Mkuu wa Wilaya ya Kigoma amesisitiza kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kukamilisha zoezi hilo kwa wakati. Amesisitiza kwamba zoezi hilo ni la Kitaifa na ni lazima likamilike mwezi Mei, 2022. Lakini pia kukamilika kwa zoezi hilo litarahisisha zoezi linalokuja la Kitaifa la Sensa ya watu na makazi. Mh. Mkuu wa Wilaya ya Kigoma pia amewashukuru wajumbe wa kamati ya uratibu wa zoezi hilo la Mfumo wa Anwani za Makazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mh. Ester Alexander Mahawe (Wa pili kutoka kulia) pamoja na viongozi wengine wakishiriki kikao kazi. Aliyesimama ni Mwenyekiti wa Kamati ya utekelezaji mfumo wa Anwani za Makazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Bi. Petronila Gwakila
Watendaji wa Kata na Vijiji, viongozi na wageni waalikwa wakishiriki kikao kazi ili kutekeleza mfumo wa Anwani za Makazi.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mh. Ester Alexander Mahawe (wa pili kutoka kulia mwenye nguo nyeupe) katika zoezi la uzinduzi wa utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwenye nyumba iliyopewa namba moja (01) katika Kata ya Mahembe.