DAGAA WA KIGOMA NI BORA ZAIDI YA KITOWEO CHOCHOTE NCHINI
Posted on: April 7th, 2017
DAGAA WA KIGOMA NI BORA ZAIDI YA KITOWEO CHOCHOTE NCHINI
Kuna baadhi ya watu wanadhani kuwa , Dagaa ni Kitoweo cha Kimaskini, kuwa kununua Dagaa Sokoni au Super Market' kwa ajili ya Kitoweo, ni dalili ya Muhusika Kuishiwa au kuwa na Bajeti Ndogo.
KAMA ukibahatika kutembelea katika masoko mbalimbali nchini bei ya Dagaa au Ndagala kama wasemavyo wa Kongomani maarufu kama Dagaa wa Kigoma mara nyingi imekuwa juu ikilinganishwa na nyama, Dagaa wengine au kitoweo chochote unachokijua nchini.
Dagaa wa Kigoma wanapatikana Ziwa Tanganyika, wanapendwa na watu wengi na sifa kubwa ya kitoweo hicho ni kutokuwa na Mchanga.
Kwa wakazi wa Mkoa wa Kigoma, wengi wanaendesha maisha yao kutokana na kuuza kitoweo hicho ambacho kimekuwa kikisafirishwa na kuuzwa katika maeneo mbalimbali nchini na nchi jirani kama za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Vijiji vya, Mwamgongo, Kagunga,Nkonkwa, Lagosa, Kibirizi na Katumbi ambavyo viko katika mwambao wa Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma ni maarufu kwa kufanya biashara hiyo ya Dagaa.
Katika vijiji hicho makundi ya wanawake na vijana wamejiajiri katika biashara hiyo na wengi wanakiri kwamba imewasaidia kuendesha maisha yao na familia zao. Mwandishi wa Makala hii alizungumza na wafanyabiashara na wavuvi ili kujua siri ya mafanikio hayo.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Salama Athumani, anasema Dagaa huandaliwa katika Mazingira Safi na kuwafanya kuwa bora zaidi. “Ni nadra mtu kula Dagaa wa Kigoma halafu wawe na mchanga na kama ikitokea ni mara chache labda mtu aliokota waliodondoka chini na kuchanganya na wengine,” anasema Salama.
UKAUSHAJI
Kwa kiasi kikubwa Dagaa huuzwa wakiwa tayari wamekaushwa lakini jamii nyingi za wavuvi awali zilikuwa zikitumia mbinu ambazo hazikuwa salama kiafya ambazo zilichangia kupunguza ubora na Soko la Kitoweo hicho kutokana na kuharibika pamoja na upotevu wake. Katika maeneo ya Afrika inakadiriwa kuwa samaki wanaoharibika kabla ya kumfikia mlaji ni kati ya asilimia 20 hadi 25 na wakati mwingine hufikia asilimia 50.
Ofisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, John Mapunda, anasema kutokana na ongezeko la Watu na Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi, Mahitaji ya samaki yameendelea Kuongezeka Siku hadi Siku, hivyo kusababisha uzalishaji samaki kutoka kwenye vyanzo vya asili kupungua kwa kasi.
TEKNOLOJIA YA KICHANJA
Shirika la Chakula Duniani (FAO), lilitoa Waraka wa Kuzingatiwa wa Uvuvi Endelevu (Code of Conduct for Responsible Fisheries) unaosisitiza umuhimu wa kupunguza upotevu wa samaki. Pamoja na waraka huo Shirika hilo lilikuwa linatekeleza mradi katika Jamii za Wavuvi wa Samaki Ndogondogo zilizoko katika Ziwa Tanganyika, nchini Burundi.
Mradi huo ulijikita katika kuleta mbinu za Gharama Nafuu za Ukaushaji Dagaa kwa Kuanika kwenye Kichanja ili kuhakikisha Kitoweo hicho kinakuwa Salama na kuwa na Soko zuri. Mbinu ambayo imeonekana kuwa na manufaa makubwa hivi sasa imesambaa hadi katika vijiji vilivyoko mwambao wa Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.
Patiasi Deo ambaye ni Mfanyabiashara katika Kijiji cha Lagosa, anasema ubora wa kitoweo hicho unatokana na uandaaji wake aliodai kuwa ni wa Kimataifa.
“Walikuja watu wakatufundisha kukausha Dagaa kwa kuwaweka katika vichanja badala ya kuanika chini. Zamani tulikuwa tunaanika chini halafu wakikauka tunawachekecha lakini mchanga ulikuwa hautoki wote, yaani ukianika chini mchanga, mvua na matope huharibu matokeo yake unaweza kujiharibia soko kwa sababu mtu akinunua akakuta wana mchanga anaweza asirudi tena kwako,” anasema Joseph.
Mfanyabiashara mwingine kutoka katika Kijiji cha Mwamgongo, Ismail Juma, anasema ukaushaji Dagaa kwa kutumia vichanja umeimarisha usafi na usalama wa Dagaa hao. “Tangu tuanze kukausha Dagaa kwenye vichanja bei imepanda na imekuwa ni faraja kwetu wafanyabiashara na wavuvi,” anasema Juma.
Juma anasema huwa wananunua Dagaa wabichi kwa Sh 12,000 kwa karai moja ambapo baada ya kukaushwa hupatikana kilo tano. Katika eneo hilo kilo moja huuzwa kati ya Sh 8,000 hadi 10,000 kutegemeana na msimu.
Kwasasa bei ya Dagaa Kigoma katika masoko ya jijini Dar es Salaam ni kati ya Sh 23,000, 25,000 kuna wakati wanafika hadi Tsh 30,000. “Kwasasa Dagaa wanapatikana kwa wingi kwa sababu huu ni msimu wake, lakini kuna wakati wanakuwa wachache kwahiyo lazima bei itakuwa juu tu,” anasema.
Ripoti ya FAO iliyotolewa mwaka juzi inayoonyesha kuridhishwa na mradi huo kwani pia umesaidia kutunza rasilimali za ziwa Tanganyika. Ofisa wa FAO Yvette Diei Ouadi, anasema waliwasaidia wavuvi kutengeneza chanja za kukausha zilizo juu kidogo na zenye kifuniko ili kuzuia mvua na kwamba baada ya muda mfupi vijiji vingine vilianza kuiga mbinu hiyo.
Kabla ya kuja mbinu hiyo asilimia 15 ya samaki waliokamatwa walikuwa wanapotea au wanaharibika wakati wa kukaushwa.
COSTECH, TAFIRI
Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI), hivi sasa wanatekeleza mradi unaolenga kutumia teknolojia nafuu na rafiki wa mazingira katika ukaushaji wa samaki katika vijiji vilivyoko mwambao wa Ziwa Nyasa.
Wastani wa tani 30,000 huvuliwa kwa mwaka kutoka Ziwa Nyasa huku upotevu wa samaki hasa wakati wa mvua hukifikia hadi asilimia 50 ya samaki waliovuliwa na hasa kwa samaki wadogo. Upotevu hutokana na desturi za ukaushaji samaki kwa kutumia moshi au kwa kuanika mchangani.
TAFIRI kwa msaada wa fedha kutoka COSTECH imeboresha makaushio ya gharama nafuu yanayotumia nishati ya Jua kwa ajili ya ukaushaji wa samaki wadogo wadogo.
Mradi huo ulianza mwaka 2013 ukiwa na lengo la kuboresha mbinu za matumizi ya Nishati ya Jua katika Kukausha Samaki kwa kutumia Makaushio au Majiko yanayotumia Nishati ya Jua.
Majiko hayo yanatumia vifaa vinavyopatikana kirahisi katika mazingira husika. Yapo makaushio ya Hema, Boksi, Shimo na Meza ya wazi ambayo hufanya Kazi kwa kuzingatia Uwezo wa Kuhifadhi Joto na Unyevu Nje na Ndani, Mwendo Kasi wa Upepo wa Nje, Kasi ya Ukaushaji na Muda wa Bidhaa Kudumu bila Kuharibika baada ya Kukaushwa.
Sampuli za Dagaa wakavu waliochakatwa zilipelekwa kwenye maabara za Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) ili kuchunguza viinilishe na madini na aina ya kaushio la hema limeonyesha kufanya vizuri zaidi ikilinganishwa na makaushio mengine.
FAIDA ZA DAGAA
Dk. Willy Sangu, anasema Dagaa ni chanzo cha madini ya chuma mwilini. “Ni chakula bora kwetu sote ambacho kinaweza kuliwa na wali, ugali, ndizi za kuchemsha, mihogo, viazi na vyakula vingine.”
Kwa ujumla Teknolojia hiyo ya Ukaushaji Dagaa ni Nafuu na imechangia Ubora wa Kitoweo hicho kuongezeka siku hadi siku na Kuboresha Kipato cha Wavuvi, Wachakataji na Wafanyabiashara ya Samaki katika Mwambao wa Ziwa Tanganyika, hivyo ni muhimu ikaendelezwa katika maeneo mengine.
KATIKA TIBA YA LISHE (DAGAA NA FAIDA ZAKE)
Tunapoangalia Umuhimu wa Dagaa na Faida zake katika Mwili wa Binadamu,Tunagundua kuwa uwe Maskini, Tajiri au Bilionea, kama Unajali Afya yako, Dagaa ni muhimu kula kuliko mapochopocho unayokula kifahari.
FAIDA KWA AFYA YA MOYO
Kama ilivyo kwa Karanga na Korosho,Dagaa nao wameonesha kuwa na Faida Kubwa kwa wenye matatizo ya Magonjwa ya Moyo. Dagaa wana virutubisho vingi na miongoni mwa virutubisho hivyo kuna kiwango kikikubwa cha Omega-3 Fatty
Acids (EPA & DHA).
Katika Tafiti nyingi za Magonjwa ya Moyo na Tiba zake, virutubisho vya Omega 3 vimeonekan kuwa Dawa au kinga kubwa sana ya Magonjwa ya Moyo. Chanzo kikuu cha virutubisho hivyo si vingine bali ni pamoja na Dagaa.
Aidha, Dagaa pia ni chanzo kizuri cha Vitamin B12, ikiwa ni chanzo kizuri cha pili baada ya maini. Vitamin hii hufanyakazi kubwa ya kuboresha ustawi wa moyo na hivyo kuwa chakula kizuri cha kumpa ahueni au kinga madhubuti mlaji dhidi ya magonjwa ya moyo.
AFYA YA MIFUPA
Dagaa ni chanzo kingine kizuri cha madini ya Calcium' yenye jukumu la kuimarisha mifupa ya mwili, lakini pia kwenye Dagaa kuna vitamin D ambayo huwa nadra sana kupatikana kwenye lishe.
Vitamin D hufanyakazi muhimu ya kuimarisha afya ya mifupa kwani ndiyo inayosaidia unyonywaji mwilini wa madini ya calcium'. Vile vile Dagaa ni chanzo kizuri cha madini aina ya phosphorus', ambayo nayo huimarisha mifupa.
DAGAA NA MARADHI YA KANSA
Kwa miaka mingi, watafiti wameona jinsi ambavyo Dagaa inavyoweza kudhibiti Seli zinazosambaza Saratani Mwilini. Hivyo Imethibitika Pasi na Shaka kuwa virutubisho vilivyomo kwenye Dagaa huweza kutoa Kinga kubwa dhidi ya Ugonjwa wa Saratani.
WAMEJAA PROTINI
Kama una upungufu wa protini mwilini,basi kula Dagaa kwani wao wana kiwango kikubwa cha kirutubisho hicho.Protini husaidia uzalishaji wa Amino acids' ambazo ni muhimu kwa uzalishaji wa chembe hai mwilini na uimarishaji wa mfumo wa kinga ya mwili (body immune system).
TAHADHARI
Wagonjwa wa figo na wale wenye matatizo ya; gout’, wanashauriwa kula Dagaa kiasi kidogo na kwa Tahadhari kubwa au kuepuka kabisa. Sababu inayotolewa ni kwamba, kama ilivyo kwa baadhi ya vyakula vingine, Dagaa huwa na vitu (Purine) ambavyo vinaweza kuwasumbua watu wenye magonjwa hayo, vinginevyo Dagaa Siyo Chakula cha kukosa kula!