UJENZI WA SOKO LA KAGUNGA WENYE THAMANI YA SH.BIL 5.6 KUCHANGIA ONGEZEKO LA MAPATO HALMASHAURI YA WILAYA KIGOMA
Posted on: December 24th, 2024HALMASHAURI ya Wilaya ya Kigoma imesaini mkataba wa kuanza ujenzi wa soko la kimkakati la Kimataifa katika Mwalo wa Kagunga Kata ya Kagunga ambalo litawezesha wafanyabiashara wazawa na Nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo DRC kufanya biashara kwa pamoja na kukuza uchumi.
Hayo yamejiri leo tarehe 24 Disemba,2024 wakati wa utiaji saini Mkataba wa ujenzi wa soko la kimkakati la kimataifa la Kagunga baina ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na Mkandarasi anayejulikana kama GOBA CONTRACTERS inayosimamiwa na Watanzania wazawa na kuongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe.Joseph Nyambwe.
Akizungumza baada ya zoezi hilo Mhe.Nyambwe amemtaka Mkandarasi aliyepewa tenda ya ujenzi wa soko la Kagunga GOPA CONTRACTERS kuhakikisha wanazingatia makubaliano ya Mkataba ili mradi ukamilike kwa wakati.
“Ni muhimu sana kwa serikali kujenga soko la kimataifa la Kagunga kwa kuwa tuna imani kubwa soko hilo litachagiza kwa kiwango kikubwa ongezeko la mapato ya halmashauri na kukuza uchumi zaidi kwa wananchi wenyeji na wafanyabiashara kutoka nchi jirani" amesisitiza Mhe.Nyambwe
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri Hiyo Bw.Linus Sikainda Amesema ujenzi wa soko hilo utagharimu Shilingi Bilioni 5.6 hadi kukamilika kwake ambapo awamu ya kwanza tayari Serikali imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 2 Ili kuanza utekelezaji wa ujenzi wa Mradi wa soko hilo.
“Tumeamua kumpa mkandarasi mzawa mradi huo, kwa kuwa nimefuatilia hatua zote na kujiridhisha kuwa ana vigezo na matarajio yetu ni kuona mradi unakidhi ubora na unakamilika kwa wakati"
Bw.Sikainda Ameongeza kuwa mradi huo utakuwa chachu ya kuongezeka mapato ya halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kutoka shilingi milioni 160 kwa mwezi hadi kufikia zaidi ya shilingi milioni 200 na hivyo kufanya halamashauri kuwa na kitega uchumi imara katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Aidha Mkandarasi aliyepewa Tenda ya Ujenzi wa soko hilo, Godfrey John Mogera kutoka kampuni ya GOPA CONTRACTERS, ameipongeza Serikali kwa kuwaamini Wakandarasi wazawa, na kwamba ni hatua muhimu katika kutekeleza miradi kwa ubora na kuhakikisha inaleta chachu ya maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.