SERIKALI YAOKOA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 60 KWENYE UJENZI WA MADARAJA YA MAWE KOTE NCHINI

Naibu Waziri kutoka OR-TAMISEMI Mhe.Zainab Katimba(Mb)amesema ujenzi wa madaraja yanayotumia teknolojia ya mawe kwa nchi nzima umeokoa zaidi ya shilingi bilioni 60 kutokana na urahisi wa upatikanaji wa malighafi na gharama nafuu za ujenzi.
Mhe.Zainab ametoa kauli hiyo leo tarehe 12 Machi,2025 wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI ilipofanya ziara ya kutembelea ujenzi wa daraja katika barabara ya Bweru-Mgaraganza yenye km 2.9 iliyojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 499.3 chini ya Wakala wa Barabara za mijini na vijijini(TARURA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma
"Teknolojia iliyotumika hapa ni ya mawe,haya madaraja ya mawe uzuri wake kwanza ni imara na yanaweza kudumu hata zaidi ya miaka 50,lakini pia ujenzi wake ni wa gharama nafuu kuliko madaraja ya zege" amesisitiza Mhe.Zainab na kuongeza:-
"Madaraja kama haya kwa nchi nzima mpaka wakati huu yapo 395 yaliyojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 24 badala ya shilingi bilioni 89.3,tafsiri yake tumeokoa zaidi ya shilingi bilioni 65,kwahiyo utaona tija ya kutumia tekolnolojia hii ya mawe"
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Justin Nyamoga(Mb) ambaye pia ni Mbunge wa Kilolo amewapongeza Watendaji mbalimbali wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwa namna wanavyosimamia kwa weledi utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ikiwemo ya Miundombinu ya barabara
Ujenzi wa daraja linalounganisha Barabara ya Bweru na Mgaraganza umewawezesha Wananchi wa Kata za Bitale na Kata nyingine za jirani kufika haraka kwenye huduma za kijamii kama hospitali na shule pamoja na kuharakisha shughuli mbalimbali za kiuchumi na biashara.