RIPOTI YA MARAFIKI WA ELIMU: UKOSEFU WA MIPAKA YA SHULE NA MATUNDU YA VYOO BADO NI CHANGAMOTO KUBWA KIGOMA
Posted on: April 2nd, 2017
RIPOTI 4 za Marafiki wa Elimu Wilayani Kigoma zimebaini kwa Ujumla Matatizo ya Ukosefu wa Mipaka ya shule na Matundu ya Vyoo kuwa ni changamoto Kubwa zinazozikabili Shule nyingi wilayani Kigoma.
Wakiwasilisha kwa Awamu Matokeo ya Utafiti Uliofanywa na Marafiki wa Elimu Wilayani hapa, Wawakilishi wa Makundi Mane yaliyotembelea Shule Kadhaa na Kukusanya Taarifa hizo katika Kikao cha Wadau wa Elimu kilichofanyika katika Ukumbi wa JOY IN THE HARVEST Manispaa ya Kigoma/Ujiji na kujumuisha Marafiki wa Elimu, Viongozi na Watumishi wa H/W KIGOMA.
''Mkutano huu ni kwa ajili ya kupokea Taarifa kutoka kwa Marafiki wa Elimu ambao awali walipewa Mafunzo juu ya Ufuatiliaji wa Uwajibikaji Jamii na baadae kwenda Kukusanya Taarifa katika shule 12 za Misingi na 8 za Sekondari ambapo makundi mane yamewasilisha Ripoti ya Kile walichokikuta katika Shule hizo’’. (Alisema Meneja Habari na Utetezi Bw. Elisante Kitulo)
Akifanya Tathmini ya Ripoti hiyo toka kwa Marafiki wa Elimu, Bw. Elisante Kitulo amewapongeza Waalimu na Vongozi wa Serikali za Mitaa kwa Ushirikiano Walioutoa katika Kufanikisha Upatikanaji wa Taarifa za changamoto zinazozikabili Shule hizo.
Katika Taarifa ya Ripoti hizo, Changamoto kubwa zilizojitokeza ni migogoro ya mipaka ambayo inazikabili shule nyingi wilayani Kigoma, swala ambalo limetajwa kuwa linatokana na ardhi ya shule nyingi kutokuwa na mipaka na kusababisha migogoro ya ardhi kati ya shule na wananchi wanaozunguka shule hizo.
Changamoto nyingine Iliyojitokeza katika Taarifa hizo ni Swala la Miundombinu ya Shule hususani Uchakavu na Uhaba wa Matundu ya Vyoo ambapo Shule nyingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma zinakabiliwa na Tatizo la Ukosefu wa Vyoo na Uhaba wa Matundi ya vyoo.
Takwimu za Taarifa za Elimu ya Msingi za mwaka 2014, Maarufu kwa jina la BEST 2014 zinaonyesha kuwa Uwiano wa Wanafunzi na Matundu ya Vyoo kwa shule za msingi Inchini ulikuwa ni 1:53 (Wanafunzi 53 kwa Tundu moja la choo) wakati Uwiano uliowekwa na Serikali ni tundu moja kutumiwa na Wanafunzi 20 Wasichana na 25 Wavulana.
Wakichangia Ripoti hiyo Wadau mbalimbali walihoji kuwa ni nani anapaswa kuwajibika kwa wanafunzi wetu kukosa huduma bora za kielimu ‘’Je ni Serikali, Uongozi wa Shule au Jamii kwa Ujumla?’’ Na kusema kuwa tatizo hili kwa sasa limekuwa Sugu katika shule za msingi kwani hali inaonyesha wazi kuwa shule nyingi za Misingi hazina vyoo vinavyokidhi Mahitaji ya Wanafunzi swala ambalo linapunguza Ufanisi wa watoto wetu kujifunza na kupata Elimu iliyobora.
Marafiki wa elimu wengine walisema kuwa ni kweli makundi hayo matatu yanawajibika katika Maendeleo ya Shule na hasa katika Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya shule, lakini moja ya chombo ambacho kimepewa mamlaka ya kusimamia uendeshaji wa shule za msingi ni Kamati za Shule. Hiki ni kikundi cha Wajumbe waliochaguliwa kwa kuzingatia Nyadhifa zao ili kusimamia Maendeleo ya Shule hizo kwa niaba ya Jamii. Waliyasema hayo huku wakirejelea Sheria ya elimu 1978, Inayosema kuwa KILA SHULE INAPASWA KUWA NA KAMATI YA SHULE.
Wengine waliyaelezea Majukumu ya Kamati hizo kuwa ni pamoja na kuandaa Mpango wa Maendeleo ya shule, kuhakikisha shule inakuwa na Miundombinu na Vifaa kamili na Bora na kutafuta vyanzo vya Fedha kwa ajili ya Ustawi na Maendeleo ya shule. Kulingana na majukumu yaliyoanishwa baadhi ya marafiki wa elimu wanashawishika kuamini kuwa ukubwa watatizo la vyoo katika shule za msingi nchini linachangia pia na kamati za shule kutowajibika ipasavyo. Baadhi walidai kuwa kamati za shule zetu zinaonekana kukosa ubunifu na weledi wa kutatua changamoto zinazozikabili shule nyingi za kata hususani tatizo la vyoo na kusubiri fedha kutoka serikalini ilhali wananchi wa Kigoma wakihamasishwa kuchangia shughuli za maendeleo huwa hawana shida.
Ukizungukia katika vijiji vingi utakuta kuna benki za matofari ambayo wananchi wamejitolea kwa maendeleo ya shule na matofari mengine yanaharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha kwa kukosekana ubunifu wa viongozi na kamati katika kutafuta vyanzo mbadala vya fedha za ujenzi’’. Alisema Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Mh. Bwami.
Aidha Mh. Bwami hakuridhishwa na namna Ripoti za Tafiti mbalimbali zimekuwa zikicheleweshwa kuwasilishwa Mahala husika kitu ambacho kimekuwa kitoa tarifa zisizoendana na Uhalisia na kusema kuwa Ripoti hizi zinazojadiliwa zinatokana na tafiti ya mwaka jana na kudai kuwa inawezekana kinachojadiliwa leo hii kimeisha patiwa ufumbuzi na sio tatizo tena kwa maeneo husika hivyo aliwataka Taasisi ya Hakielimu kuwa na utaratibu wa kuwasilisha mapema matokeo ya tafiti pundu tuu zinapopatikana ili serikali na wahusika waweze kuchukua hatua kwa haraka Zaidi.
Makamu huyo pia alikiri kuwa taarifa za ukosefu wa madawati ni za kweli katika halmashauri yake ingawa wao kama viongozi wanampango wa kulimaliza tatizo hizo kwa kuwa halmashauri inamisitu ambayo itatumika kupasua mbao za madawati licha ya taarifa hiyo lakini bado hata taarifa za halmashauri zinaonyesha kuwa tatizo hilo lipo.
HakiElimu ni shirika la Hiari linalolenga kuona Jamii yenye Uwazi, inayozingatia Haki, Demokrasia na inatoa Elimu bora kwa wote. Shirika hilo limekuwa likifanya hivyo kwa kuwezesha Jamii kupata habari, kubadili shule na uundaji wa sera, kuchochea Ubunifu wa Mijadala ya Umma, kufanya utafiti yakinifu, Uchambuzi wa sera na kushirikiana na wadau ili kuendeleza Manufaa ya pamoja kwa kuzingatia haki ya Jamii. HakiElimu inawasaidia Wanainchi kujua haki na wajibu wao kwa kuwapa Taarifa mbalimbali ili waweze kuchukua hatua za kuboresha Elimu.
Halmashauri ya wilaya ya Kigoma ina jumla ya shule za Misingi 109, kati ya hizo shule za serikali ni 106 na Binafsi 3, Vituo vya kuendeleza Waalimu TRC’s vilivyopo ni 3. Idadi ya Waalimu waliopo ni 1,231. Idadi ya wanafunzi waliopo ni 56,661 kati ya hao Wavulana ni 28,171 na Wasichana ni 28,445. Hali ya uandikishaji wa wanafunzi Darasa la Kwanza kwa mwaka 2016 ilikuwa ni Wanafunzi 9,551 kati ya hao Wavulana ni 4,659 na Wasichana 4,892 sawa na 100.76%. Ufaulu wa wanafunzi katika Mtihani wa Darasa la Saba kwa Mwaka 2016 umeongezeka na kufikia 79.78% sawa na ongezeko la 24.69% kwa Mwaka 2015.
Halmashauri imeendelea kupata Fedha za Uedeshaji wa shule kupitia Mpango wa Elimu Bila Malipo ambapo Jumla ya TZS 215,139,000 zimepokelewa kutoka serikali kuu kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2016, Fedha hizo zilipokelewa Mashuleni pia Halmashauri imetekeleza mkakati wa kupunguza Tatizo la madawati toka 8,963 hadi kufikia 3,945. Idara ina mahitaji ya Miundombinu mbalimbali kama ifuatavyo; Madarasa 1,412, yaliyopo 670 na upungufu 742, Nyumba za walimu mahitaji 1,412, zilizopo 196 na upungufu 1,216.
02/04/2017
Habari na. Shaban Akapela (Afisa Habari KDC) anapatikana 0763112532 Email : juniorkapera@gmail.com