DCC KIGOMA DC YAPITISHA MCHAKATO WA MGAWANYO WA KATA

Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kimepitisha kwa kauli moja mchakato wa kugawanya kata za Simbo, Kalinzi na Mkongoro katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwa lengo la kusogeza huduma za kijamii karibu zaidi na makazi ya Wananchi.
Maazimio hayo yameridhiwa na Kamati hiyo leo Machi 13, 2025 kupitia kikao kilichoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe.Dkt.Rashid Chuachua na kuhudhuriwa na Wajumbe kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Katika Mgawanyo huo mpya wa maeneo ya Utawala kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, kupitia Kata ya Simbo zinatarajiwa kuanzishwa Kata nyingine ya Nyamoli itakayokuwa na Vijiji vya Nyamoli Kimbwela na Kaseke huku Kata ya Simbo ikisalia na Vijiji vya Simbo, Machazo na Kasuku.
Aidha kutokana na kata ya Kalinzi inatarajiwa kuanzishwa kata mpya ya Mkabogo itakayokuwa na Vijiji vya Mkabogo na Milinzi na Kata ya Kalinzi kusalia na Vijiji vya Kalinzi, Mlangala na Matyazo.
Kadhalika kupitia kata ya Mkongoro inatarajiwa kuanzishwa kata mpya ya Nyamhoza itakayokuwa na Vijiji vya Nyamhoza Nyabigufa na Mkwanga huku Kata ya Mkongoro ikisaliwa na Vijiji vya Mkongoro na Chankele.
Mgawanyo huo mpya wa maeneo ya Utawala unatarajiwa kuongeza Kata za Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kutoka 16 zilizopo sasa hadi kufikia idadi ya Kata 19.