HALMASHAURI YA WILAYA YA KIGOMA YAPIGA HATUA UTOAJI WA CHAKULA SHULENI

Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma imepiga hatua katika kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe shuleni, ambapo jumla ya shule 141 kati ya 151 za msingi na sekondari tayari zinatoa chakula kwa wanafunzi sawa na zaidi ya 93% ya shule zote.
Hayo yamebainika katika kikao cha Kamati ya Lishe ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwa Robo ya Tatu kuanzia Mwezi Januari-Machi, kujadili utekelezaji wa shughuli za Afua za Lishe.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe.Dkt. Rashid Chuachua,Afisa Tawala Bi.Dora Buzaile amepongeza hatua hiyo na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi, walimu na jamii ili kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi anayesoma akiwa na njaa.
Amesema Mafanikio hayo yamechangiwa na utekelezaji wa mikakati mbalimbali inayolenga kuhamasisha ushiriki wa wazazi na jamii kupitia utoaji wa elimu ya lishe kwa wazazi katika vikao rasmi, pamoja na kuanzishwa kwa sheria ndogondogo zinazowataka wazazi kuchangia huduma ya chakula.
Bi.Dora ameongeza kuwa ushirikiano kati ya idara ya elimu na idara ya kilimo umeimarika, ambapo mbegu zimegawiwa kwenye shule mbalimbali huku elimu ya kilimo ikitolewa ili Wanafunzi waweze kupata chakula kupitia mashamba na bustani za shule.
"Lengo kuu ni kuhakikisha kila mwanafunzi wa Kigoma anapata lishe bora, afya njema, na mazingira salama ya kujifunzia ili kuimarisha ufaulu na maendeleo ya elimu kwa ujumla" amesisitiza Bi Dora
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Halmashauri ya kigoma Bi. Sarah Kibindu amesema,hii ni hatua ya kupongezwa na ya kujivunia kwa kila mdau wa Lishe ambaye ametoa mchango wake na kuhimiza wadau wote kuendelea kushirikiana kwa ajili ya kuwa na kizazi chenye afya na maarifa.
Takribani Miezi minne imetimia tangu Mkuu wa Mkoa wa kigoma Mhe.CGF(Rtd) Thobias Andengenye kuwaagiza Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kila shule inatoa chakula cha mchana kwa wanafunzi.
https://www.instagram.com/p/DJdttzAteJh/?igsh=bGxlc2UzeDlod25i