WAKULIMA WA ZAO LA MCHIKICHI WATAKIWA KUTUMIA MBEGU BORA ILI KUONGEZA UZALISHAJI NA KUKUZA KIPATO

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe.Dkt.Rashid Chuachua amewataka wazalishaji wa zao la Mchikichi kuendelea kutumia mbinu bora za uzalishaji ikiwemo matumizi ya mbegu bora ili zao hilo lizalishwe kwa wingi na kuongeza tija.
Mhe.Dkt.Chuachua ametoa kauli hiyo leo tarehe 16 Aprili,2025 wakati alipotembelea wazalishaji wa zao la Mchikichi katika maeneo ya Gereza la Kwitanga na kambi ya Jeshi la kujenga Taifa JKT Bulombora katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Dkt.Chuachua ametumia fursa hiyo kuwasihi Mamlaka ya Utafiti wa Mbegu nchini (TARI) kuendelea kutoa elimu kwa wakulima wa zao la Mchikichi na kusambaza mbegu bora ili wakulima waweze kuzalisha Mchikichi kwa wingi huku akisisitiza matumizi ya mbegu ijulikanayo kama TENERA ili kuvuna mazao mengi na bora.
Akizungumza kwa niaba ya Uongozi wa Gereza la Kwitanga SP.Johnbosco Ngema amesema pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kilimo cha zao la mchikichi ameomba kuboreshwa kwa miundombinu ya umwagiliaji ili kuongeza mazao mengi zaidi na kuachana na kutegemea mvua pekee.
Naye Kiongozi kutoka Kikosi cha Jeshi la kujenga Taifa JKT Bulombora Meja Msumi ameomba Mamlaka zinazohusika kuwawezesha vifaa maalum vya umwagiliaji ili waweze kumwagilia shamba lao lenye michikichi zaidi ya 1000 na kuongeza kiwango cha uzalishaji wa zao hilo.
Zoezi alilofanya Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe.Dkt.Rashid Chuachua la kutembelea na kukagua maendeleo ya uzalishaji kwenye mashamba ya zao la Mchikichi ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa kuhusu uboreshaji wa kilimo cha Mchikichi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla.