DC.DKT. CHUACHUA ASISITIZA WAZAZI KUWAWEZESHA WANAFUNZI KUPATA CHAKULA SHULENI

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe.Dkt.Rashid Chuachua amewataka Wazazi kuchangia chakula shuleni ili kuwawezesha wanafunzi kupata mlo wakati wakiendelea na masomo.
Dkt.Chuachua ameyasema hayo leo tarehe 12 Machi,2025 wakati wa Kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa Afua za Lishe cha Robo ya Pili kuanzia Mwezi Oktoba hadi Disemba kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Amesema ifikapo tarehe 15 Machi,2025 Wanafunzi kwenye shule zote wanapaswa wawe wameanza kuhudumiwa chakula ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe.Thobias Andengenye alilolitoa hivi karibuni.
Aidha Dkt.Chuachua amewasisitiza Watendaji wa Kata mbalimbali kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha zoezi hilo huku akiongeza kuwa Mzazi yeyote atakayebainika kukwamisha suala la huduma ya chakula hatavumiliwa.
"Ukiona kundi la Wazazi linashindwa kuchangia chakula shuleni kwaajili ya watoto wao,tambua kuna mzazi kinara katika kundi hilo anayewapotosha wenzake,tuchukue hatua" amebainisha Dkt.Chuachua
Akitoa taarifa katika kikao hicho Mratibu wa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Bi.Sarah Kibindu amesema wamezingatia maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya na kueleza kuwa Halmashauri itaendelea kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa Mkataba wa Lishe ngazi ya Halmashauri ili kuepukana na changamoto ya udumavu na utapiamlo.