MOHAMED MCHENGERWA ATOA MIEZI MITATU KUKAMILISHA KITUO CHA AFYA KAGUNGAA
Posted on: August 13th, 2024Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI,Mohamed Mchengerwa ametoa muda wa miezi mitatu kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kutoa fedha milioni 300 ili kukamilisha ujenzi wa Kituo cha afya cha Kagunga katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma ili kuwaondolea adha wananchi ya kufuata huduma za afya nchi jirani ya Burundi.
Agizo halo limetolewa na waziri huyo wakati akiongea na wananchi pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo la Utawala wa Halmashauri ya Wilaya ya kigoma na kuridhishwa na kasi ya ujenzi huo.
Amesema hahitaji kuona wananchi wa Tanzania wakiendelea kupata huduma nchini Burundi badala yake wananchi wa wa nchi hiyo ndio waje kupata huduma nchini kutokana na kuboresha huduma bora za afya
Hoja ya kumalizika kwa Kituo hicho ilitolewa na Mwenyekiti wa halmashauri ya Kigoma Joseph Nyambwe ambaye alisema ukosefu wa kituo cha afya katika kata hiyo ni changamoto kwa wakazi hao ambapo inawalazimu kuingia gharama zaidi wakifuata huduma za afya nchi jirani ya Burundi
Hata hivyo baadhi ya Wananchi walipata fursa ya kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwa ni pamoja na mrundikano wa wanafunzi katika shule ya msingi Mahembe, ukosefu wa hosteli Shule ya sekondari Mgawa na kuomba serikali kuzipatia ufumbuzi.
Katika ziara hiyo Waziri Mchengerwa mbali na kuongea na watumishi wa umma pia ametembelea na kukagua ujenzi wa daraja la kilembela katika kijiji Cha Mgaraganza mradi unayosimamiwa na TARURA, ujenzi wa shule mpya eneo la Kazegunga na ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri ya wilaya ya Kigoma.