MEMKWA KUSAIDIA WALIOKOSA ELIMU KWA MFUMO RASMI
Posted on: March 21st, 2023Na Mwandishi Wetu:
Wadau wa elimu, Viongozi ngazi ya kata na Vijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wametakiwa kuihamasisha jamii kujiunga na Mpango wa elimu mbadala (MEMKWA) kwa Watoto Walioikosa. Yamesemwa hayo na Afisa Elimu ya Watu Wazima Mkoa wa Kigoma Ndugu. Hawamu Tambwe wakati wakimalizia mafunzo ya siku 5 ya kuwajengea uwezo Walimu wa MEMKWA, Maafisa Elimu wa Kata na Walimu wakuu yaliyofanyika kuanzia Machi 17-21, 2023.
Pichani juu: Picha ya pamoja ya Washiriki wa Mafunzo.
Mafunzo hayo yamefanyikia ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma yakihusisha Maafisa Watendaji wa Kata, Maafisa Elimu wa Kata, Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Walimu wakuu na Walimu wa MEMKWA chini mradi wa Elimisha Mtoto unaofadhiliwa na Shirika la UNICEF
Mwezeshaji wa mafunzo ya MEMKWA Kitaifa kutoka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Ndugu. Dastan Msamada amesema elimu hiyo hufundishwa stadi za Kusoma, Kuandika na kuhesabu pamoja na Stadi za maisha, Falsafa ya Ujasiriamali, na stadi za ufundi kwa lengo la kuchangia Maendeleo ya Taifa pindi anapohitimu masomo. Amesema elimu ya MEMKWA hutolewa kwa kundi rika umri wa miaka 8-13 na kwa vijana walio na umri 14-18 na baadae hujiunga katika mfumo wa elimu rasmi kwa kufanya mtihani wa Darasa la Nne na la Saba
Pichani juu: Mwezeshaji wa Kitaifa ndugu. Dastan Msamada (Kushoto) kutoka Taasisi ya Elimu ya watu wazima akiongea na washiriki wa mafunzo.
Afisa elimu Watu wazima wa Msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma ndugu. Reinfrid Fidelis Nyeshahu amesema vituo vya MEMKWA vipo Kumi (10) kwenye Kata Tano (5) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Akifunga mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Ndugu. Jabir Timbako amesema jamii inapaswa kuhakikisha watoto wote waliokosa elimu kwa mfumo rasmi wanapata fulsa hii ya elimu mbadala pasipo kikwazo chochote ili kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Pichani juu: Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ndugu. Jabir Timbako (aliyesimama) akiongea na washiriki wa mafunzo na kufunga mafunzoo hayo.
Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Nchini inataka kupata idadi kubwa ya Watanzania walioelimika, wanaopenda kujielimisha, ili waweze kuchangia Maendeleo ya Taifa. Serikali imetoa fursa kwa watoto waliokosa elimu katika mfumo rasmi kupata elimu hiyo kupitia Mpango wa elimu mbadala (MEMKWA)