KIGOMA DC YATOA MKOPO SH.MIL 209,816,000 KWA VIKUNDI VYA WANAWAKE,VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe.Dkt.Rashid Chuachua amevitaka vikundi vya Wanawake,vijana na watu wenye ulemavu kutumia fedha za mikopo ya 10% inayotolewa na Halmashauri itumike kwaajili ya kutekeleza miradi waliyoombea mikopo na si vinginevyo.
Dkt.Chuachua amebainisha hayo leo tarehe 5 Machi,2025 wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya kiasi cha Shilingi Milioni 209,816,000 kwaajili ya mikopo ya asilimia 10 kwa vya Wanawake,vijana na watu wenye ulemavu na ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Amesema Serikali inatenga fedha hizi kwa mujibu wa Sheria na taratibu ili kuviwezesha vikundi vyenye sifa kupata mikopo kwa wakati huku akiitaka Halmashauri kusaidia kurasimisha vikundi hivyo na kuvipatia kipaumbele kwenye zabuni za miradi ya Halmashauri ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Jabir Timbako amesema Halmashauri itaendelea kutenga fedha asilimia 10 kwa mujibu wa sheria na kwamba vikundi vyilivyopewa mkopo vimekidhi vigezo vya kupatiwa mkopo na kuvitaka vikundi hivyo kurejesha fedha hizo ndani ya kipindi kilichopangwa ili mikopo iwafikie na watu wengine.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini Mhe.Makanika ameeleza kuwa zoezi la utoaji mikopo kwa vikundi vyenye sifa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kupitia Serikali ya awamu ya sita inayobainisha kutoa kipaumbele cha mikopo kwa vikundi vya Wanawake vijana na watu wenye ulemavu ili kuwawezesha Wananchi kujikwamua kiichumi.
Aidha katika hafla hiyo wafanyabiashara wadogowadogo 54 wamekabidhiwa vitambulisho vya ujasiriamali vinavyodumu kwa muda wa miaka 3 kwa gharama ya sh.20,000/= huku zoezi la uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara likiendelea na utoaji wa usaidizi kwa wafanyabiashara wadogowadogo kujisajili kwenye mfumo ili kupatiwa kitambulisho.
Hata hivyo vikundi vyote vilivyokabidhiwa mkopo vimepatiwa mafunzo kuhusu ujasiriamali,Uongozi na utawala wa vikundi, usimamizi wa fedha,uibuaji na uandishi wa andiko la mradi wa kutoka kwa wataalam ili kuhakikisha fedha hizo zilizotolewa zinaongeza tija na kukuza kipato cha vikundi na kipato cha mtu mmojammoja.