KATIBU MKUU CCM AAGIZA UJENZI WA KITUO CHA AFYA NA CHA POLISI -MWANDIGA
Posted on: August 5th, 2024Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Emanuel Nchimbi amemuagiza Waziri wa mambo ya ndani,Hamad Masauni na Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa, kujenga kituo cha afya na kituo cha polisi katika kata ya Mwandiga kabla ya uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika 2025.
Katibu Mkuu Emanuel Nchimbi akizungumza na Wananchi wa mwandiga
Nchimbi amesema hayo akihutubia mkutano wa wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini uliofanyika kata ya Mwandiga,halmashauri ya wilaya ya Kigoma akiwa kwenye ziara ya kichama mkoani Kigoma.
Agizo hilo limetokea baada ya baadhi ya wananchi kushikilia mabango yenye ujumbe wa kuiomba serikali kuwajengea vituo hivyo kutokana na umuhimu wake katika jamii na ujenzi wa taifa.
Amesema wananchi wanaomba kujengewa kituo cha polisi ni wema hivyo jitihada za dhati zifanyike kwaajili ya ujenzi huo.
Akizungumzia upande wa kituo cha afya amesema michakato isikwamishe ujenzi wa kituo hicho na utekelezaji wake ufanyike kwa haraka
Hata hivyo katikbu mkuu amewashukuru wananchi waliojitokeza katika mkutano huo kwa namna walivyoishukuru serikali kwa uboreshaji wa huduma kwa wananchi na kuzitaka wizara husika kuendelea kufanya kazi ili kukamilisha miradi yote ya maendeleo iliyoahidiwa kwa wananchi ikiwemo kusogeza Nishati ya umeme kwa wananchi wanaishi vijijini.
Katika hatua nyingine Nchimbi amekipongeza Chama cha Mapinduzi na serikali ya mkoa Kigoma kwa kusimamia utekelezaji wa miradi inayotokana na fedha ya serikali kiasi cha shilingi trilioni 11.4 zilizotolewa mkoani humo katika kipindi cha miaka mitatu .
Amesema anafurahishwa na mienendo ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwamba ipo katika viwango vizuri na hivyo kuwataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais Samia
Wakizungumza baadhi ya wananchi wa kata hiyo, Amina Salimwe mzaliwa wa Mwandiga amesema endapo kituo cha afya kitajengwa kitapunguza adha ya akina mama wajawazito ya kutembea umbali mrefu kwaajili ya kujifungua hususani katika vituo vya afya na hospitali zilizopo manispaa ya Kigoma Ujiji.
Salimwe ameiomba pia serikali kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya cha Kagunga ili kianze kufanya kazi na kupunguza changamoto ya wananchi wa eneo hilo kwenda kutibiwa katika nchi jirani ya Burundi
Kwa upande wa kituo cha polisi Said Ramadhani amesema kituo hicho kitakapopatikana kitapunguza adha za uhalifu na utoaji taarifa kwa msaada wa usalama hasa kwa nyakati za usiku.
Katika ziara yake Kigoma Katibu Mkuu wa CCM amevuna wanachama zaidi ya 250 kutoka vyama vya upinzani