KASSIM MAJALIWA AWATAKA WANANCHI KUHAKIKISHA WANAOANDIKISHWA NI RAIA WA TANZANIA
Posted on: July 22nd, 2024Waziri mkuu Kassim Majaliwa ametoa kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuwatambua na kutoa taarifa za uwepo wa watu ambao si raia wa Tanzania katika kila kituo cha uandikishaji.
Waziri Majaliwa ameyasema hayo katika uzinduzi wa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura uliofanyika katika viwanjwa vya Kawawa vilivyopo manispaa ya Kigoma Ujiji.
Amesema mwananchi ndiye mtu wa kwanza kutambua nani ni mtanzania na nani si mtanzania katika maeneo wanaoishi hivyo kuwe na ushirikiano baina yao na jeshi la uhamiaji ili kutambua wasio na sifa ya utanzania ili wasijiandikishe katika daftari hilo na kufanya zoezi hilo kufanyika kwa ufanisi mkubwa.
“Watanzania lazima tuwe wazalendo, upigaji kura ni kwa sisi watanzania, tunachagua viongozi watakaoliongoza taifa la Tanzania, tunachagua viongozi ambao watakuja kuwa viongozi wa mitaa yetu na vitongoji vyetu, kwanini kuruhusu mtu wa nje aje atupigie kura? Atatuamlia ambavyo sisi hatutaki, kwahio tusiruhurusu mtu yoyote kutoka nje ajiandikishe katika daftari la mpiga kura” Alisema Majaliwa.
Amesema kila mtanzania asimamie zoezi hilo kwa uadilifu, kwa kutoa taarifa sahihi za raia anayetaka kujiandikisha ambaye si mtanzania kwani zoezi hilo ni la watanzania pekee na si vinginevyo.
Vile vile amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuweka mawakala watakaosimamia zoezi hilo kutoka katika kijiji husika kwakuwa ndio wanaowafahamu wananchi wa maeneo yao na hivyo kuwa rahisi kutambua ambao hawana sifa za kuandikishwa kama raia wa Tanzania.
“Naomba mawakala wote muwe wazalendo na makini kuangalia kila anayekuja kuboresha taarifa zake na kufuatilia namna anavyohojiwa kwakuwa maelezo yake yanaweza kutusaidia kutambua aliye raia na asiye raia” Alisisitiza Majaliwa.
Hata hivyo amewataka watendaji na wote watakaohusika katika zoezi la uandikishaji kutumia lugha nzuri, kutoa maelekezo mazuri ,na kutekeleza wajibu huo kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazotolewa na tume na kwamba wahakikishe zoezi hilo linakamilika pa bila kuwa na dosari yoyote