KAMATI ZA HUDUMA ZA MIKOPO ZIMETAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUFUATA KANUNI NA TARATIBU ZA UTOAJI WA MIKOPO
Posted on: October 4th, 2024Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kigoma, Jabir Timbako amezitaka kamati za huduma ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ngazi ya kata kusimamia mchakato wa upatikanaji wa vikundi vinavyokidhi kupata mikopo ya asilimia 10 yenye lengo la kuwainua kiuchumi.
Bw.Timbuko amesema hayo leo tarehe 22 Oktoba,2024 katika mafunzo ya kamati zinazojumuisha wataalamu kutoka ngazi ya Kijiji na Kata wakiwemo, Watendaji wa Kata na Vijiji, Maafisa Ustawi wa Jamii,Maafisa Ugani, Waratibu Elimu, pamoja na Polisi Kata kwa lengo la kujifunza kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, mafunzo yaliyofanyika katika mji mdogo wa Mwandiga.
“Mmeteuliwa kwa barua kuwa sehemu ya kamati ili kutekeleza majukumu yaliyopo ambayo ni muhimu kwa ujenzi wa taifa, tunaomba mkatimize majukumu yenu kwa kufuata mwongozo na kanuni za mwaka 2024, hakikisheni mnapata vikundi vyenye sifa ya kupata mikopo kwa robo hii na si vinginevyo” Amesema Timbako
Aidha Kaimu Mkurugenzi amezitaka kamati hizo kutoa elimu kwa vikundi ambavyo havitakuwa vimekidhi vigezo vya kupata mkopo kwa sasa ili wanakikundi wakamilishe taratibu zote zinazotakiwa kwaajili ya kupata mkopo kwa wakati mwingine.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya jamii George Vangesauli amesema kamati zinapaswa kuwa wazi kuielezea jamii taratibu zinazotakiwa kwa vikundi vinavyopaswa kupata mikopo ili kuondoa malalamiko kwa wale watakaokosa mkopo kutokana na kushindwa kuwa na sifa zinazotakiwa.
Halmashauri ya wilaya ya Kigoma imetenga jumla ya shilingi milioni 200,380,614/= katika Robo ya Pili ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 kwaajili ya mikopo ya asilimia 10,hata hivyo wananchi wanakumbushwa kuwa mwisho wa kutuma maombi ya mkopo huo ni tarehe 31,Oktoba 2024.