KAMATI YA SIASA YA CCM MKOA WA KIGOMA YARIDHISHWA KASI YA UTEKELEZAJI WA MIRADI KIGOMA D.C

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kigoma Mhe.Jamal Tamimu amesema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa Miradi mbalimbali ikiwemo ya elimu na afya kwa kuzingatia Ilani ya CCM kwenye maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Mhe.Jamal amesema hayo leo tarehe 27 Februari,2025 wakati kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Kigoma ilipotembelea na kukagua utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo katika Kata za Mkigo,Nyarubanda, Mkongoro,Mwandiga,Simbo na Kidahwe kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma
Mhe.Jamal akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe.Dkt.Rashid Chuachua,Katibu Tawala Mhe.Mganwa Nzota, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Mwl.Chiriku Hamisi Chilumba pamoja na wataalamu mbalimbali wamekagua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Amali katika kijiji cha Kasange unaogharimu shilingi milioni 603 ambao ujenzi wake upo katika hatua ya kupaua.
Miradi mingine iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba 4 vya madarasa na matundu 6 ya vyoo katika shule ya msingi Ukombozi kwenye Kata ya Mkongoro unaogharimu shilingi milioni 118 na ujenzi wa jengo la Maabara,jengo la chumba cha upasuaji na wodi ya Mama na Mtoto kwenye kituo cha Afya cha Simbo wenye gharama ya shilingi milioni 631.
Mwenyekiti wa CCM Mhe.Jamal pamoja na kumpongeza Mhe.Mkuu wa Wilaya ya Kigoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma amesema lengo lao ni kuona Ilani ya CCM inatekelezwa kikamilifu kwa kuhakikisha Miradi yote ambayo Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameleta fedha inatekelezwa na kuwanufaisha wananchi kwa kuwapatia huduma karibu zaidi na makazi yao.
"Mhe.D.C na Mkurugenzi Mtendaji kwakweli mnafanya kazi nzuri,hiki ndio hasa ambacho Serikali yetu inataka,Mhe.Mama Samia anapenda anapotoa fedha aone kazi kweli zinafanyika"amesisitiza Mhe.Jamal
Miradi mingine iliyotembelewa na kukaguliwa na Ujenzi wa Tanki la Maji la ujazo wa lita laki 3 uliopo katika kijiji cha Mkigo wenye gharama ya shilingi bilioni 1.6 ,mradi wa Barabara ya Mwandiga -Chankere unaogharimu shilingi milioni 475 katika Kata ya Mwandiga pamoja na mradi wa ujenzi wa Kituo cha kupokea na kupooza umeme katika eneo la Kidahwe unaogharimu jumla ya shilingi bilioni 5.