HATUA ZA AWALI UJENZI KITUO CHA AFYA MWANDIGA ZAANZA-DED ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Mwl.Chiriku Hamisi Chilumba ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa kituo kipya cha Afya cha Mwandiga kinachojengwa katika eneo la Bigabiro kwa thamani ya shilingi milioni 250.
Hayo yamedhihirika leo tarehe 10 Julai,2025 wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo alipotembelea na kukagua hatua za awali za ujenzi wa kituo cha Afya Mwandiga ambacho kinatarajiwa kuhudumia Wakazi zaidi ya Elfu 20 kutoka Kata ya Mwandiga na maeneo ya jirani.
Ujenzi wa kituo cha Afya Mwandiga umechagizwa na kiasi cha fedha cha sh.Mil.250 kilicholetwa na Serikali kuu ambapo itatumika kujenga jengo la wagonjwa wa nje,choo cha matundu 5 na miundombinu mingine.
Ujenzi wa kituo hiki cha Afya ni mwendelezo wa dhamira ya dhati ya Serikali ya kusogeza huduma za afya karibu zaidi na makazi ya watu na kuwaondolea Wananchi adha ya kutembea mwendo mrefu kufuata huduma ya afya.