MIKOPO YENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 122 YATOLEWA KWA VIKUNDI VYA WANAWAKE, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU.
Posted on: March 30th, 2023Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma inaendelea kutenga na kupeleka mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na vikundi vya watu wenye ulemavu kwa mujibu wa sheria na kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo. Mikopo hii inatokana na asilimia 10 ya Mapato ya ndani yanayokusanywa na Halmashauri kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato. Taarifa iliyosomwa na Afisa Maendeleo ya Jamii Bi. Minza Edward mbele ya Mgeni rasmi Mh. Salum Hamisi Kalli ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, imesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma imefanikiwa kutenga na kupeleka mikopo kiasi cha shilingi 122,492,583 kwa vikundi 11 ambapo vikundi vya wanawake 4, vijana 4 na vikundi vya watu wenye ulemavu 3. Aidha kiasi cha shilingi 45,514,583 zimetokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya mwezi Julai 2022 hadi Januari 2023 na kiasi cha shilingi 76,978,000 ni fedha zinazotokana na marejesho ya mikopo iliyokopeshwa miaka ya nyuma.
Pichani juu: Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mh. Salum Hamisi Kalli (mwenye Suti Nyeusi) aliyekuwa mgeni rasmi wa hafla ya utoaji mikopo.
Pichani juu: Mfano wa Hundi ya shilingi Milioni 122,492,583 iliyotolewa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Pichani juu: Mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mh. Salum Hamisi Kalli (mwenye Suti Nyeusi) akikabidhi cheti kwa mmoja wa kiongozi wa kikundi vijana.
Pichani juu: Mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mh. Salum Hamisi Kalli (mwenye Suti Nyeusi) akikabidhi cheti kwa mmoja wa kiongozi wa kikundi cha wanawake.
Akiongea katika hafla hiyo, mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mh. Salum Hamisi Kalli amewasisitiza wanufaika wa mikopo hiyo kuitumia mikopo katika shughuli iliyokusudiwa na kikundi. Mgeni rasmi pia amesisitiza vikundi hivyo kufanya marejesho ya mikopo hiyo ili na wananchi wengine pia wanufaike.
Vikundi hivyo vinajishughulisha na biashara ya mazao ya nafaka, biashara ya Mawese, Ufugaji wa kuku na mbuzi, utengenezaji wa sabuni, mashine ya kusaga, biashara ya samaki na dagaa na kiwanda kidogo cha utengenezaji wa chaki.
Pichani juu: Ni baadhi ya wakuu wa idara na vitengo pamoja na mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mh. Salum Hamisi Kalli (aliyekaa mwenye Suti Nyeusi)
Pichani juu: Afisa Maendeleo Bi. Minza Edward (kushoto aliyesimama) akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi Mh. Salum Hamisi Kalli, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma
Pichani juu: Ni vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wakimsikiliza mgeni rasmi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma ndugu. Jabir Timbako amesema wataendelea kutenga pesa na kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa mujibu wa sheria na kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo hiyo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Mh. Albogast Ndiyuze amesisitiza lengo la mikopo hii ni kuwainua wananchi kiuchumi. Amesema mikopo hii ni sehemu ya kile ambacho tumekusanya kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato na ikiwemo ushuru wa biashara zinazofanywa na wananchi hao.
Hafla hiyo ya utoaji mikopo imehudhuliwa pia na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma ambaye amewakilishwa na Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM)