Halmashauri imeendelea na hatua za uboreshaji wa maeneo ya makazi na biashara, katika kipindi cha mwaka 2015/16 jumla ya viwanja 15 vilipimwa katika kijiji cha Kidahwe na vibanda 400 vilipimwa katika eneo jipya la mnada lililoanzishwa na Halmashauri katika kijiji cha Kamara. Halmashauri ilikuwa na mkakati wa kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyote 46, mpaka kufikia Juni, 2016 vijiji ambavyo vimefanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi ni 25, sawa na 52.1% ya vijiji vyote. Zoezi la ugawaji wa vijiji wakati mwingine limekuwa ni changamoto kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi uliofanyika katika vijiji vilivyogawanywa.
Halmashauri ya wilaya ya kigoma kwa kushirikiana na shirika la BTC imekuwa ikitekeleza mradi wa BTC ulioanza mwaka 2013 na kumalizika 2016. Mradi wa BTC ulifanikiwa kutoa mafunzo ya ufugaji bora wa nyuki katika vijiji 6 vya Bitale, Nkungwe, Mahembe, Mgaraganza, Simbo, na Kidahwe. Pamoja na utoaji wa mafunzo BTC wameweza kujenga kituo cha uzalishaji wa Malkia wa nyuki, kituo hicho kimejengwa katika kijiji cha Kidahwe.
Halmashauri ina jumla ya vikundi 20 vya ufugaji nyuki vyenye jumla ya mizinga 904 kati ya hiyo 788 ni ya kienyeji/ Asili na 116 ni ya kisasa. Uzalishaji wa asali kwa mwaka kwa vikundi vilivyopo unakaribia kufikia kiasi cha lita 308.