WATENDAJI WA VIJIJI WATAKIWA KUBAINI MAENEO YA UWEKEZAJI NA UMILIKI WAKE KATIKA MAENEO YAO
Posted on: April 15th, 2024Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kigoma Chiriku Chilumba amewaomba watendaji wa serikali za mitaa, vijiji na kata kubaini maeneo ya uwekezaji katika maeneo yao, yanayomilikiwa na serikali au mtu binfasi ili kuondoa migogoro ya ardhi pindi utetekelezaji wa miradi ya maendeleo utakapoanza katika maeneo husika.
Amesema hayo katika kikao kazi cha halmashauri hiyo kilichohusisha viongozi wa ulinzi na usalama, walimu wakuu shule za msingi na sekondari, watendaji wa kata na viiji, wenyeviti wa mitaa na vitongoji,makatibu tarafa pamoja na viongozi kutoka taasisi mbalimbali kwa lengo la kupeana taarifa za utendaji kazi.
Amesema kubainika kwa maeneo hayo mapema kutasaidia miradi ya maendeleo kuanza kwa wakati kwakuwa hatua zote za awali zitakuwa zimechukuliwa kikamilifu na kuruhusu miradi hiyo kuanza bila changamoto kwaajili ya ustawi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.
Aidha mkurugenzi Chilumba amewataka walimu wakuu kudhibiti utoro mashuleni na kuhakikisha wanafunzi wanaanza masomo yao katika muda uliopangwa huku akitilia mkazo suala la chakula shuleni ili kudhibiti utoro huo.
Pamoja na hayo mkurugenzi amewaomba viongozi wa serikali za mitaa kutoa taarifa za dharura zinazotokea katika maeneo yao ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa kwajili ya kuwasaidia wahanga kinyume na kukaa na taarifa za namna hiyo kwa muda mrefu.
“Katika kipindi hiki cha mafuriko, naomba kuwe na mawasiliano ya haraka, itakuwa haileti maana kupata taarifa za uharibifu baada ya siku tatu au nne wakati viongozi wa serikali za mitaa wapo, tutoe taarifa kwa wakati ili kuokoa waliofikwa na dharura” Amesema Chilumba.
Katika kikao hicho ambacho kimeongozwa na mkuu wa wilaya ya Kigoma Salum Kalli, amewataka watendaji hao kufanya majukumu yao kikamilifu na kuondoa changamoto zozote zinazo ikabili jamii ikiwemo kufunga nyumba za kulala za wageni zinazojihusisha na biashara ya ngono pamoja na kubaini wahamiaji haramu waliopo katika maeneo yao na kupata taarifa zao kikamilifu.