WANANCHI KIJIJI CHA CHANKERE WAJENGA VYUMBA 2 VYA MADARASA KWA NGUVU ZAO

- Wananchi wa kijiji cha Chankere Kata ya Mkongoro kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wameanza ujenzi wa vyumba 2 vya Madarasa vya Shule ya Sekondari kwa nguvu zao ili kuwaondolea watoto adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata elimu.
Hayo yamebainika leo tarehe 10 Julai,2025 wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Mwl.Chiriku Hamisi Chilumba akiwa ameambatana na wataalam kutembelea ujenzi wa vyumba vya Madarasa katika kijiji cha Chankere.
Akizungumza na baadhi ya Viongozi wa Kijiji hicho pamoja na wananchi DED Chilumba amefurahishwa na namna ambavyo Wananchi wa Kijiji hicho wamejitolea kuanza ujenzi wa vyumba vya Madarasa na kusisitiza kuwa hatua hiyo imerahisisha shughuli ya kutafuta fedha ili kukamilisha ujenzi wa shule hiyo.
Amesema pamoja na Halmashauri kuwa na majukumu mengi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali,utekelezaji wa shughuli hizo huwa rahisi na kupewa kipaumbele kwenye maeneo ambayo Wananchi wameonesha nia na kujitolea nguvu zao.
Wakizungumza baada ya Mkutano huo Viongozi wa Kijiji hicho wamesema wanafurahi kuona kiu yao ya muda mrefu ya kuwa na shule ya Sekondari katika kijiji chao inakwenda kutimia na hatimaye kuwapunguzia watoto wao madhila ya kutembea umbali mrefu kwenda kufuata huduma ya Elimu.