WALIMU WAKUU KIGOMA WANOLEWA UONGOZI NA USIMAMIZI WA UJIFUNZAJI NA UFUNDISHAJI

Walimu Wakuu wa shule za msingi na Waratibu wa Jumuiya za kujifunza (JzK) Mkoani Kigoma wamepatiwa Mafunzo ya Uongozi na usimamizi wa Ujifunzaji na Ufundishaji ili kuendana na dira,dhima na misingi ya maadili ya shule kwa lengo la kuwa na uelewa wa pamoja katika utekelezaji wa shughuli kwenye mazingira ya kazi.
Mafunzo hayo yanayotekelezwa na mradi wa Shule Bora unaofadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia mfuko wa UK Aid yamefanyika kwa siku 3 katika ukumbi wa Bwalo la shule ya Sekondari ya Mwandiga iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Mwezeshaji wa Mafunzo hayo Bi.Chrisencia Victor amesema Mafunzo haya yatawawezesha walimu Wakuu kwenda kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia usimamizi thabiti wa Rasilimali za shule pamoja na kukabiliana na changamoto ya KKK kwa Wanafunzi ili kuwaongezea Wanafunzi maarifa zaidi na kukuza ufaulu.
Kwa upande wake Mwl.Ramadhan Thabiti ameelezea malengo ya Jumuiya za kujifunza(JzK) kuwa ni kujengeana uwezo kwa urahisi katika ngazi mbalimbali hasa kwenye masuala ya Uongozi na usimamizi wa Ujifunzaji na Ufundishaji na kutatua changamoto zinazokabili Kata moja moja kwa kuzipatia ufumbuzi na kusonga mbele.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na Walimu Wakuu 54 wa shule za msingi kutoka katika Halmashauri 8 za Mkoa wa Kigoma huku Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma ikihusisha Jumuiya za kujifunza (JzK)kutoka ambazo ni Kazi,Kidamte,Nyamki,Simbo,Mashujaa wa Elimu,Mwanya na Mwamgongo.