WAKAZI ZAIDI YA ELFU 20 MWANDIGA KUNUFAIKA NA MRADI WA KITUO KIPYA CHA AFYA

Wakazi zaidi ya Elfu 20 kutoka Kata ya Mwandiga na maeneo ya jirani wanatarajiwa kuondokana na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya afya baada ya Serikali kutenga kiasi cha sh.Mil.250 kwaajili ya ujenzi wa kituo cha Afya cha Mwandiga.
Hayo yamebainika leo tarehe 28 Juni,2025 wakati Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe.Dkt.Rashid Chuachua aliposhiriki zoezi la usafi na uchimbaji wa Msingi pamoja na Wananchi katika eneo la Bigabiro ambako unafanyika ujenzi wa kituo cha Afya cha Mwandiga katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Akizungumza baada ya zoezi hilo Dkt.Chuachua amesema mradi huu utakua ni kielelezo cha kazi kubwa anayofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya afya ambayo itawawezesha wananchi kupata huduma karibu zaidi ili maisha yao yaendelee kustawi.
"Leo tunaweka kituo cha Afya hapa,akina Mama waliokuwa wanatembea umbali mrefu watafika hapa na watapata huduma zote,vituo vya Afya vya Sasa ni vya kisasa na huduma zote ambazo unazipata kwenye hospitali ya Wilaya kuna wakati utazipata kwenye Kituo cha Afya" ameeleza Dkt.Chuachua
Amesema ni muhimu Wananchi kushiriki kufanya kazi zilizo ndani ya uwezo ili wawe na umiliki na mradi lakini pia kuona na kuunga mkono juhudi za Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Mwl.Chiriku Hamisi Chilumba amebainisha kuwa kiasi cha fedha cha sh.Mil.250 kimeletwa ndani ya mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo itatumika kujenga jengo la wagonjwa wa nje,choo cha matundu 5 na miundombinu mingine.
Mwl.Chilumba ameongeza kuwa ushiriki wa wananchi katika kuchimba msingi na usafi wa mazingira kumewezesha kuokoa kiasi cha Shilingi milioni 2 ambazo zitaelekezwa kutekeleza shughuli nyingine za Ujenzi.