WAHE.MADIWANI WAMPONGEZA DED CHILUMBA KWA KASI KUBWA YA MAENDELEO NA UTENDAJI THABITI KIGOMA DC
Posted on: December 12th, 2024Waheshimiwa Madiwani kutoka Kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wamempongeza Mkurugenzi Mtendaji Bw.Chiriku Hamisi Chilumba kwa kasi kubwa ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo na Uongozi thabiti ndani ya kipindi kifupi cha uwepo wake.
Wah.Madiwani wametoa kauli hiyo leo tarehe 11 Disemba 2024,wakati wa Kikao cha Baraza la Kata kwaajili ya kupitia na kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo kwa Robo ya Kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025, kilichofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wakiwasilisha taarifa zao,Wah.Madiwani wamesema wanashuhudia mabadiliko makubwa kwenye utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo lakini pia usimamizi thabiti unaowezesha Miradi mingi kukamilika ndani ya muda uliopangwa jambo linalowawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi na karibu zaidi na maeneo yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Bw.Chiriku Hamisi Chilumba amewashukuru waheshimiwa Madiwani kwa pongezi na kusisitiza kuwa mabadiliko hayo yanatokana na ushirikiano mkubwa baina yake na Wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma ambao wamekua wakitekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Aidha DED Chilumba amewashukuru Waheshimiwa Madiwani kwa namna wanavyotekeleza majukumu kwenye Kata zao,na kuwaasa kuendelea kushirikiana kwa kutoa mawazo na ushauri ili shughuli za maendeleo kwenye Kata moja moja na Halmashauri yote kwa ujumla zitekelezwe kwa ufanisi na kwa viwango vinavyostahili
.