UBORESHAJI MIUNDOMBINU SHULE YA SEKONDARI MGAWA WATAJWA KUPUNGUZA UKATILI WA KIJINSIA,WANANCHI WA MAHEMBE WASHUKURU
Posted on: December 19th, 2024Shirika la Maendeleo la Ubelgiji Enabel kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania linatarajia kuboresha miundombinu katika shule ya Sekondari ya Mgawa iliyopo katika Kata ya Mahembe kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma ili kuwaondolea Wanafunzi adha ya kutembea mwendo mrefu kufuata huduma ya elimu na kupunguza ukatili wa kijinsia.
Hayo yamebainika leo tarehe 17 Disemba,2024 wakati wa mkutano wa majadiliano ngazi ya jamii na utambulisho wa Mradi wa 'Wezesha Binti' uliofanyika katika eneo la Mahembe Sokoni kwa lengo la kujadili utatuzi wa changamoto ya ukatili wa kijinsia pamoja na kuwainua kiuchumi watoto wenye Umri wa miaka 14-29.
Akizungumza katika mkutano huo Mwezeshaji kutoka Shirika la Enabel Bw.Marcel Kato amesema wameamua kuboresha miundombinu katika shule za Sekondari ili kuwawezesha Wanafunzi hasa wa kike ili waweze kubaki shuleni na kupata muda mwingi zaidi wa kujikita na masomo yao.
"Tumebahatika Sekondari yetu ya Mgawa na yenyewe iko kwenye mpango wa kuboreshwa kwa kujengewa miundombinu kwaajili ya wanafunzi hasa kwa wanafunzi wa kike kwa kuwawezesha kubaki shuleni na kupunguza changamoto zinazompelekea binti asiweze kumaliza elimu yake ya Sekondari na kuendelea mbele"amesisitiza Bw.Kato
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mahembe Kati Bw.Dunia Ahmad amesema "mabinti wengi wanapata mimba kutokana na mazingira lakini miundombinu ikiboreshwa watakua na nafasi nzuri ya kujisomea,lakini pia vijana wetu wengi wanatoka katika familia zisizo na uwezo,hata wakifaulu familia zinashindwa kuwaendeleza,hii ni changamoto"
Akizungumzia hali ya Ukatili wa kijinsia katika Kata ya Mahembe Mtendaji wa Kata hiyo Bi.Sheila Mahamudu amesema uwepo wa kamati za kukabiliana na ukatili wa kijinsia umepunguza kwa kiasi kikubwa vitendo hivyo na kwamba wanaendelea kutoa elimu ili kuijengea jamii uelewa mpana wa athari za ukatili wa kijinsia hasa katika ngazi ya familia.
Mradi wa 'Wezesha Binti' unaofadhiliwa na Shirika la maendeleo la Ubelgiji kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania na kutekelezwa katika Halmashauri tano za Mkoa wa Kigoma umekamilisha hatua ya majadiliano ngazi ya jamii na utambulisho katika kata tano za Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma ambazo ni Kidahwe,Kalinzi,Mkongoro,Mwamgongo na Mahembe.