TASAF YA MKWAMUA KIUCHUMI MKAZI WA KIJIJI CHA NYABIGUFA
Posted on: May 21st, 2024Musin Japhari mkazi wa kijiji cha Nyabhigufa kata ya Mkongoro halmashauri ya wilaya ya Kigoma ni mmoja kati ya wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (PSSN) chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambaye ameweza kupata manufaa makubwa kutokana na mpango huo.
Akizungumza wakati wa ziara ya waandishi wa habari wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kanda ya magharibi amesema licha ya pesa kidogo anayopata kutoka TASAF amefanikiwa kujenga nyumba ya bati kupitia kilimo cha machungwa, mapapai na michikichi ambayo alianzisha baada ya kupata pesa hiyo.
Akizungumzia bustani ya machungwa aliyoanza kulima mwaka 2014 amesema amefanikiwa kupata pesa nyingi toka alipoanza kuvuna zilizomuwezesha kumudu elimu ya watoto, kubadili mlo na kununua mahitaji ya watoto ya shuleni pamoja na nyumbani.
“Sikuwa na uwezo wa kununua viatu vya shule vya watoto kila walipohitaji, sare na mabegi ilikuwa changamoto kupata, hata kupata pesa za kununua nguo mara kwa mara kwaajili ya watoto kubadilisha ilikuwa taabu, ila toka nimeanza kuuza machungwa napata pesa ya kutosha kukidhi mahitaji madogo madogo” amesema Japhar.
Amesema kwa msimu mmoja anauza machungwa mara mbili, na kwa msimu uliopita alipata fedha zaidi ya laki saba (700’000/-) na kwa msimu huu mpaka sasa ameshauza zaidi ya laki nne (400,000/-).
Japhari amesema anatarajia kuongeza idadi ya miche kutoka 68 iliyopo sasa mpaka kufikia 200 ili aweze kuongeza uzalishaji na kupata kipato zaidi, amewashauri wanufaika wote wa TASAF ambao wanapata pesa na kula waziingize katika uzalishaji ili ziwasaidie zaidi na kwa muda mrefu.
“Mafanikio sio kuanza na mtaji mkubwa, mafanikio ni kuanza na kipato kidogo na kisha kukikuza, hivyo pesa kidogo wanayopata kutoka TASAF waitumie kama mtaji wa kufanya biashara, kufuga na hata kulima ili kuongeza kipato na hatimae kuwa huru kiuchumi” Ameshauri Japhari.
Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri ya Kigoma George Vangesauli afisa ustawi wa jamii amesema jumla ya wananchi 6764 wananufaika na mpango wa kunusuru kaya masikini katika wilaya hiyo.
Amesema kwa pindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan zaidi ya shilingi bilioni mbili zimetolewa kwaajili ya wanufaika wa mpango huo katika nyanja za elimu, na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya ukarabati wa miundombinu ya barabara na uchimbaji wa visima huku shilingi zaidi ya milioni 386 zikitolewa kila awamu.
Vangesauli amefafanua kuwa kwa kipindi cha mwaka 2014 hadi 2024 wanufaika 20 wamehitimu mpango wa TASAF na sasa wanaishi huru kiuchumi wakiendesha biashara zao wenyewe, wakiishi kwenye nyumba zao na wakiwa na uwezo wa kusomesha watoto katika ngazi za juu za elimu.
Amesema hatua hiyo inatoa chachu kwa serikali kuingiza wanufaika wapya wanaoishi katika umasikini ili waweze kunufaika na mpango huo na hatimae wawe huru kiuchumi.