SERIKALI KUENDELEA KUTOA RUZUKU KWA MBEGU ZA MAZAO MBALIMBALI KUONGEZA TIJA NA UZALISHAJI

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe.IGP(Mst )Balozi Simon Sirro amesema Serikali imedhamiria kuendelea na mpango wa ruzuku kwa mbegu za mazao mbalimbali ili kuhakikisha wakulima wanaongeza tija ya mavuno na kuwa na usalama wa chakula na kujiongezea kipato.
Balozi Sirro ametoa kauli hiyo leo tarehe 8 Agosti wakati akihitimisha Kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane kwa Kanda ya Magharibi yaliyofanyika katika viwanja vya Fatma Mwasa Ipuli Mkoani Tabora.
Maadhimisho hayo yaliyopambwa na burudani mbalimbali yamehudhuriwa na mamia ya Wananchi pamoja na Viongozi wa Serikali kutoka Mikoa ya Kigoma pamoja na Mkoa wa Tabora,wadau mbalimbali na Taasisi za umma na binafsi.
Amesema wakulima wa kanda ya Magharibi wanapaswa kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kujisajili na kuhuisha taarifa zao ili kuweza kuendelea kunufaika na mpango wa mbolea za ruzuku zinazotolewa ili kufanya kilimo cha tija na kujihakikishia Usalama wa chakula.
Aidha Mhe.Balozi Sirro amewataka Wafugaji kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la chanjo ya Mifugo na kuelekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa za mikoa ya Tabora na Kigoma kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mpango wa chanjo na utambuzi wa mifugo katika maeneo yao ili kuiepusha Mifugo na magonjwa ya hatari.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Wizara ya Kilimo na Mifugo Twalib Njohore amesema Wizara imedhamiria kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao kwa kutoa pembejeo za ruzuku na mbegu bora kwa wakulima.
Maonesho ya Nane kwa mwaka 2025 yenye Kaulimbiu "Chagua Viongozi bora kwa maendeleo endelevu ya Kilimo Mifugo na Uvuvi"yalianza tarehe 1 Agosti,2025 na kuhitimishwa leo tarehe 8 Agosti,2025.