RC SIRRO ASISITIZA WANANCHI KUTUMIA SEKTA YA KILIMO NA FURSA ZA BIASHARA KUINUA UCHUMI NA KUONGEZA KIPATO

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe.IGP(mst) Balozi Simon Sirro amewataka Wananchi wa Mkoa wa Kigoma kuendelea kuvutia wawekezaji katika sekta ya kilimo,ufugaji na fusra za Biashara ili kukuza kipato cha Wananchi na kukuza ustawi wa maisha.
Balozi Sirro ametoa kauli hiyo leo tarehe 11 Julai,2025 wakati akizungumza na Wananchi na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwenye mwendelezo wa Ziara yake ya kutembelea Halmashauri mbalimbali za mkoa wa Kigoma.
Mhe.Sirro amesema kwa kutumia Wataalamu wa kilimo na Biashara katika Halmashauri,Wananchi wanaweza kujifunza mbinu mbalimbali zitakazowawezesha kukuza shughuli hizo na kuongeza tija kwaajili ya manufaa ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla
Aidha Mhe.Balozi Sirro amewataka watumishi wa umma kutimiza wajibu wao kwa Wananchi kwa kutekeleza majukumu waliyopewa ili kuwasaidia Wananchi na kutatua changamoto zao huku akisisitiza kutumia muda wa kazini vizuri kwaajili ya kuwahudumia Wananchi.
Katika hatua nyingine Mhe.Balozi Sirro amekagua ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma iliyopo eneo la Mahembe huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu na kuongeza idadi ya watumishi ili Wananchi wapate huduma kwa wakati na kwa ufanisi.
"Sisi kama Serikali tutaona namna gani tutaongeza wataalam wa Afya,ili Wananchi wa Kigoma wasipate adha lakini pia tutaona namna ya kutafuta fedha kwaajili ya kukamilisha baadhi ya miundombinu ikiwemo chumba cha kuhifadhia maiti"amesema Balozi Sirro
Hii ni Ziara ya Kwanza kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe.IGP(Mst)Balozi Simon Sirro katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma baada ya kuteuliwa hivi karibuni na Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan