MKUU WA WILAYA YA KIGOMA ATOA WITO WA UZALENDO KATIKA KULINDA MIPAKA YA NCHI

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Mhe. Dkt.Rashid Chuachua, ametoa wito kwa wananchi wa Kata ya Mkigo kuwa wazalendo kwa kushiriki kikamilifu katika kulinda mipaka ya nchi, huku akisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu rasmi kwa wageni wanaoingia nchini.
Dkt.Chuachua ametoa mwito huo wakati Akihutubia Wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mkigo wakati wa ziara yake ya yenye lengo la kusikiliza na kujibu kero za wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma
Amesema kuwa uzalendo ni msingi muhimu wa kulinda uhuru na usalama wa taifa, na hivyo kila mwananchi anapaswa kuwa mlinzi wa mipaka kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama
.“Watanzania ni watu wakarimu. Mgeni akija mkaribishe, lakini lazima afuate utaratibu. Usalama wa nchi lazima ulindwe na Watanzania wenyewe. Haiwezekani watu kutoka nchi nyingine waingie bila kufuata taratibu.”amesisitiza Dkt.Chuachua na kuongeza kuwa;
“Fuateni utaratibu. Uzalendo wa nchi yetu ni muhimu kuliko kitu kingine chochote. Tuwe walinzi wa mipaka yetu,”
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amekemea vikali vitendo vya ubakaji na ulawiti vinavyofanywa na baadhi ya watu wasio na maadili, na kuwataka wazazi kuwa mstari wa mbele kuwalinda watoto wao dhidi ya vitendo hivyo.
“Wazazi mnatakiwa kuwa makini. Kuna watu hawapendi maendeleo, kazi yao ni kuharibu maisha ya watoto wetu. Tushirikiane kuwalinda watoto dhidi ya hawa maadui wa jamii,” amesisitiza Dkt.Chuachua
Huu ni mwendelezo wa Ziara za Mkuu wa Wilaya ya Kigoma kwenye Kata mbalimbali ili kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili Wananchi ambapo amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha hatua madhubuti zinachukuliwa ili kero zinazohusu migogoro ya ardhi, Maji,Umeme,afya na Elimu zinapungua na kumalizwa kabisa.