JAMII YATAKIWA KURIPOTI VITENDO VYA UKATILI
Posted on: March 8th, 2024Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ameionya jamii kuachana na tabia za kumaliza mashauri ya vitendo vya ukatili wa kijinsia nje ya mfumo wa sheria kwasababu yoyote ile.
Amesema kumalizana na kesi hizo kienyeji bila kufuata sheria na taratibu za nchi kunasababisha ukomavu na usugu wa vitendo hivyo.
“Watoto wetu wanaofanyiwa vitendo vya kikatili huwezi kuwalinganisha na kitu chochote hata wazazi waamue kuchukua pesa, au mifugo ili kuachana na kesi licha ya maumivu watoto wanayokuwa wameyapitia, tuache kuwaumiza watoto wetu na tutoe taarifa za vitendo hivyo kwenye vyombo vya sheria’ Amesema Andengenye.
Ameongeza kuwa asilimia 60 ya matukio ya unyanyasaji wa kijinsia hufanyika katika ngazi ya familia huku kukiwa hakuna hatua zozote za kisheria zinazochukuliwa dhidi ya watuhumiwa jambo linalosababisha vitendo hivyo kukithiri katika jamii
Aidha Andengenye amesema ili kufikia kasi ya mabadiliko ya kimkoa katika nyanja za uchumi, kisiasa na kijamii ametoa wito kwa wakurugenzi kuimarisha utaratibu wa usimamizi wa shughuli za kielimu hasa kuelekeza nguvu katika masuala ya ya usawa wa kijinsia kwa lengo la kuleta usawa katika jamii.
Amewaelekeza watendaji hao wa halmashauri kuendelea kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo katika kutekeleza mpango wa taifa wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake.
Hata hivyo amewaasa wanawake kote mkoani kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ili waweze kutoa mawazo na mchango wao katika kukuza uchumi wa jamii