MKUU WA MKOA WA KIGOMA AITAKA JAMII KUBADILI MTAZAMO KATIKA MALEZI
Posted on: May 21st, 2024Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ametoa wito kwa wazazi kuwahimiza watoto wao kufanya kazi ili wakue katika misingi ya uwajibikaji.
Ametoa wito huo leo tarehe 15 Mei 2024 wakati wa Kongamano la kilele cha Maadhimisho ya siku ya Familia ambayo kimkoa yamefanyika katika Halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji.
Amesema ili kutekeleza hilo ni muhimu wazazi waaminiane na kusaidiana majukumu ya malezi kwa kutoa muda kwa watoto wao kijamii ili kujenga urafiki na upendo miongoni mwao
Naye Afisa ustawi wa jamii Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma George Vangesal amesema kumekuwa na ongezeko la vijiwe vya wanaume katika maeneo mbalimbali mkoani humo hali inayosababisha mzigo wa malezi kumuangikia Mwanamke na kufanya suala la malezi kuwa gumu.
Vangesal amesema ni muhimu kila mmoja katika familia na jamii afanye kazi na kutimiza wajibu wake katika suala zima la malezi.
“Wazazi wanaposhindwa kutimiza wajibu wao wanasababisha watoto waingie katika matukio ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia hivyo kila mtu afanye kazi na kutimiza wajibu wake ili kunusuru Mustakabari wa maisha ya watoto”. Amesema Vangesal
Naye Chiriku Chilumba mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kigoma amesema jamii inapaswa kuunganisha nguvu kwa pamoja katika malezi mazuri ya watoto ili kupata taifa lililo bora.
Amesema suala la malezi ya watoto ni ajenda endelevu ambayo kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kulifanyia kazi, kwenye ngazi ya familia, katika vikao na mikutano ni muhimu kuendelea kulizungumzia kwa manufaa ya taifa.