MADIWANI WAIPA KONGOLE KIGOMA DC KUPAA KWA MAPATO

Waheshimiwa Madiwani wa Baraza la Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya hiyo kwa ongezeko la mapato ya ndani yanayowezesha kutekeleza shughuli za Maendeleo kwa haraka na ufanisi.
Hayo yamebainika leo tarehe 30 Mei,2025 wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani kwa Robo ya Tatu ya mwaka kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo uliopo eneo la Mahembe.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Mhe.Joseph Nyambwe amesema hatua madhubuti zilizochukuliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Mwl.Chiriku Hamisi Chilumba zimewezesha Halmashauri kukusanya zaidi ya sh.Milioni 150 kwa mwezi na kupelekea Halmashauri kukusanya zaidi ya sh.Bilioni 1.5 kwa mwaka.
Wakizungumza wakati wa Kikao hicho Wahe.Madiwani wameeleza kuridhishwa kwao na utendaji kazi wa wataalam hususan wa Idara ya Fedha kwa kubuni vyanzo mbalimbali na kusimamia ukusanyaji wa mapato unaorahisisha utekelezaji wa shughuli za Miradi ya maendeleo kwenye Halmashauri.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Linus Sikainda ametumia fursa hiyo kuwashukuru Wah.Madiwani kwa usimamizi mzuri na ushirikiano wanaoendelea kuuonesha huku akiahidi kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili shughuli zote zitekelezwe kwa wakati na kwa ufanisi.