KIGOMA D.C &KAKONKO D.C WABADILISHANA UZOEFU UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO

Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma zimejizatiti kuendelea kuwa na mashirikiano kwenye kubadilishana uzoefu katika kutekeleza miradi mkubwa ya kimkakati pamoja na miradi mingine ya maendeleo.
Hayo yamedhihirika wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Mwl.Chiriku Hamisi Chilumba pamoja na baadhi ya Wataalam walipofanya Ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katika ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Kigoma D.C pamoja na wataalam wamepata fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kwenye ujenzi wa ukumbi wa kisasa ambao umeanza kujengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kwa gharama ya Sh.Bilioni moja.
Ziara hii ya kutembelea na kujionea ujenzi wa ukumbi wa kisasa ni hatua muhimu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma ambayo inatarajia kuanza ujenzi wa ukumbi wa kisasa katika mwaka wa fedha 2025/2026 ambao utatumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo vikao pamoja na mikutano.
Aidha DED Mwl.Chilumba pamoja na wataalam wameweza kutembelea mradi wa ujenzi wa soko lililojengwa kwa fedha za mapato ya ndani kiasi cha sh.Mil 368 lililoko katika mji wa Kakonko hali kadhalika na ujenzi wa nyumba za Wakuu wa Idara na nyumba ya Mkurugenzi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji,Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Bw.Linus Sikainda amesema Ziara hiyo imekuwa ya mafanikio makubwa kwakuwa imewajenga na kuwapatia uzoefu mpya pamoja na kuwaongezea ufanisi kwenye utekelezaji wa miradi ya Kimkakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Ndaki Stephano amesema huu ni mwanzo mpya wa mashirikiano na kusisitiza kuwa kubadilishana uzoefu kunajenga mahusiano na kuimarisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa manufaa ya Wananchi katika Halmashauri wanazoziongoza.