HALMASHAURI YA WILAYA YA KIGOMA YAZINDUA ZOEZI LA CHANJO YA KUKU DHIDI YA MAGONJWA HATARI

Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma imezindua rasmi zoezi la chanjo ya kuku kwa lengo la kukabiliana na magonjwa hatari yanayowakumba hususan mafua, mdondo na ndui ili kuwawezesha wafugaji kutekeleza ufugaji wenye tija.
Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 03 Julai 2025, ukiwa umeongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Ndg. Jabil Timbako, ambaye pia amekabidhi jumla ya dozi 70,000 za chanjo kwa Maafisa Mifugo waliopo katika kata mbalimbali, tayari kwa kuanza utekelezaji wa zoezi hilo kwa wananchi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Ndg. Timbako amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kuhakikisha afya ya mifugo inaimarika, sambamba na kuinua kipato cha wananchi wanaojihusisha na ufugaji wa kuku.
"Chanjo hii ni kinga muhimu inayowalinda kuku dhidi ya magonjwa makubwa matatu na ni hatua ya kuunga mkono juhudi za wananchi katika kujikwamua kiuchumi kupitia ufugaji wa kuku," amesema Ndg. Timbako.
Zoezi hilo linatarajiwa kufanyika katika vijiji na kata zote ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, kwa usimamizi wa karibu wa wataalamu wa mifugo
ambapo Wananchi wametakiwa kushiriki kikamilifu kwa kupeleka kuku ili wapate chanjo hiyo muhimu, huku wito ukitolewa kwa viongozi wa vijiji na mitaa kushirikiana kuhakikisha elimu na uhamasishaji unawafikia wafugaji wote.