DED CHILUMBA ATOLEA UFAFANUZI HATUA ZITAKAZOONGOZA MCHAKATO WA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA
Posted on: October 18th, 2024Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Bw.Chiriku Hamisi Chilumba ametolea ufafanuzi hatua zitakazoongoza mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuanzia zoezi la Uandikishaji kwa lengo la kuhakikisha Uchaguzi unakua huru na wa Haki kwa mujibu wa Sheria.
Msimamizi wa Uchaguzi Bw.Chilumba ametoa maelezo hayo leo tarehe 18 Oktoba,2024 kwenye kikao baina yake na Viongozi wa vyama mbalimbali vya Siasa kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma eneo la Mahembe mkoani Kigoma.
Akizungumzia zoezi la uapishaji wa Mawakala wa vyama vya Siasa Bw.Chilumba amesema Uapishaji utakua endelevu kadiri Mawakala wapya watakavyokuwa wanaletwa na vyama vya Siasa na kusisitiza kuwa Mawakala wanapaswa kuapishwa kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yao.
Aidha ameeleza kuwa kuanzia tarehe 26 Oktoba,2024 hadi tarehe 1 Novemba,2024 kutafanyika zoezi la Wagombea kuchukua fomu na kurudisha huku akibainisha kuwa ukomo wa Viongozi walioko Madarakani utakua tarehe 19 Oktoba,2024 kwa mujibu wa kanuni za Uchaguzi.
Hata hivyo Bw.Chilumba ameendelea kuwasisitiza Wananchi wote wenye sifa kushiriki katika hatua zote za Uchaguzi ikiwa ni pamoja na kujiandikisha kwenye Orodha ya Wapiga Kura na kuwahimiza kujitokeza kwa wingi kutumia haki yao ya kupiga Kura kwenye Uchaguzi ifikapo tarehe 27 Novemba,2024.