DC DKT.CHUACHUA AONGOZA ZOEZI LA USAFI SIMBO AHIMIZA LIWE ENDELEVU

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe.Dkt.Rashid Chuachua amewataka Wananchi kuwa na tabia ya kufanya usafi mara kwa mara ili kuhakikisha mazingira yanalinda Afya ya Binadamu.
Dkt.Chuachua ametoa Rai hiyo leo tarehe 03 Juni,2025 wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira ulioambatana na zoezi la usafi kwenye Kituo cha Afya cha Simbo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
"Mazingira ni kitu cha msingi sana,tunachofanya hapa ni kukumbushana kuwa sio tu mazingira ya Kituo cha Afya yanapaswa kuwa safi lakini hata mazingira ya maeneo tunayoishi,usafi wa mazingira lazima uanzie nyumbani;tuyatunze mazingira yetu na tuyalinde"amesema Dkt.Chuachua
Dkt.Chuachua ameongeza kuwa kila Mwananchi kwenye kaya ahakikishe uwepo wa choo kizuri na kuwepo na eneo la kuhifadhi na kuchoma taka ili kujiepusha na maradhi hatari yanayotokana na kuzaliana kwa vimelea vinavyotokana na uchafu wa mazingira.
Aidha Dkt.Chuachua amesema Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma ina bahati ya kuwa na uoto wa asili na hivyo ni jukumu la kila Mwananchi kulinda na kuhifadhi misitu kwakuwa ndiyo inayoleta uhai wa ardhi na kusababisha mvua kwaajili ya mazao.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Simbo Mhe.Neema ameishukuru Serikali kwa kujenga mradi wa Kituo cha Afya ambao unawawezesha Wananchi kupata huduma karibu na makazi hayo huku akiwasisitiza Wananchi kuendelea kulinda mazingira ya Kituo hicho kwa kufanya usafi mara kwa mara.