D.C DKT CHUACHUA AWAHAKIKISHIA WANANCHI MGARAGANZA UTATUZI WA KERO ZINAZOWAKABILI

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Mhe.Dkt. Rashid Chuachua, amewahakikishia wananchi kuwa Serikali imedhamiria kuondoa kero mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ya migogoro ya ardhi,elimu,afya, Maji na umeme ili waweze kutekeleza shughuli zao bila bughudha.
Dkt.Chuachua amesema hayo wakati alipokuwa akisikiliza kero za Wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mgaraganza katika Kata ya Kagongo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma uliolenga kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili.
Amesema kero mbalimbali ambazo zimewasilishwa kwake zimesikilizwa, kupokelewa na kwamba baadhi yake tayari zimeanza kushughulikiwa ipasavyo kupitia wataalam wa Sekta za elimu,Maji,Umeme pamoja na ardhi.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya wataalamu kutoka idara zinazohusika wametolea ufafanuzi baadhi ya kero na kueleza kuwa hatua madhubuti zimeanza kuchukuliwa kwa Serikali kuanza kutenga fedha kwaajili ya Uboreshaji wa Miundombinu ikiwemo ya Maji na umeme.
Kuhusu migogoro ya ardhi na mipaka katika kijiji hicho Dkt. Chuachua amemuagiza Afisa Ardhi wa Wilaya kushughulikia suala hilo ndani ya siku saba ili kurejesha hali ya utulivu na mshikamano miongoni mwa wananchi na kuendelea kutekeleza shughuli zao za kila siku kwa utulivu.
Aidha Mkuu wa Wilaya ametumia fursa ya Mkutano huo kuwaeleza wananchi umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwezi Oktoba mwaka huu, huku akiwataka kupuuza propaganda na kasumba potofu za kisiasa zinazoweza kuvuruga amani na mshikamano katika kijamii.
“Wananchi shirikianeni na viongozi wenu katika kujenga kijiji chenu. Serikali yenu ipo pamoja nanyi kuhakikisha mnapata huduma stahiki,” amesisitiza Dkt. Chuachua.
Ziara hiyo imepokelewa kwa shukrani na matumaini makubwa na wakazi wa Kijiji cha Mgaraganza, wakieleza kuwa ni hatua chanya ya maendeleo na usikivu wa serikali kwa wananchi wake.