Halmashauri ya wilaya ya Kigoma kwa sehemu kubwa inategemea kilimo kama shughuli kuu ya kiuchumi katika kujiongezea kipato na chakula. Mazao makuu ya biashara yanayolimwa ni Kahawa na Michikichi, kwa upande wa mazao ya chakula ni Mahindi, Mihogo, Maharagwe, Viazi vitamu, Ndizi na Karanga. Aidha Taasisi zinazoshirikiana na Halmashauri katika shughuli za kilimo ni kama: JaneGoodall Institute – Uhifadhi wa Mazingira na Kilimo Mseto; TACRI – Utafiti zao la Kahawa; Kanyovu – Chama cha Ushirika zao la Kahawa (M); Seed Change – Uzalishaji Miche bora ya Kahawa; Gombe National Park – Kilimo cha Mihogo.
Takwimu zinaonyesha mavuno yamefikia jumla ya tani 339,349.79 kwa mazao ya Mahindi, Mpunga, Muhogo, Ndizi na Viazi Vitamu ambazo zitatoa tani 230,599.89 za wanga na upande wa mazao ya mikunde mavuno ni tani 10,889.84 ambazo zitatoa tani 2.79 za utomwili (protini). Mahitaji ya chakula kwa Halmashauri ya wilaya ya Kigoma ni tani 57,861.09 za wanga na tani 4,895.94 za utomwili hivyo kuna ziada ya tani 172,738.8 za wanga na upungufu wa tani 4,250.88 za utomwili (protin). Upungufu huu wa utomwili utafidiwa kwa upatikanaji wa mazao ya samaki, dagaa na mifugo (kuku, mbuzi, kondoo na ng’ombe.) pamoja na mazao ya mikunde yanayolimwa mabondeni kipindi cha kiangazi.
Halmashauri inahamasisha Wananchi Kuunda vikundi vya kiuchumi na vyama vya ushirika kwa lengo la kupata Masoko ya Pamoja kwa ajili ya kuuza mazao yao kwa bei nzuri na upatikanaji wa mikopo toka Taasisi za fedha kiurahisi kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi.